KOCHA mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema kuwa, matokeo ya mchezo wao uliopita dhidi ya Tanzania Prisons, yamewaongezea kitu katika hesabu zao za kuwamaliza Al Merrikh ya Sudani, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba na Al Merrikh wanatarajia kucheza mchezo wao wa marudiano wa kundi A Jumanne ijayo, mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, huku wakiwa na kumbukumbu ya suluhu kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Machi 6.
Juzi Jumatano, Simba walilazimika kusubiria mpaka dakika ya mwisho ya mchezo kuweza kusawazisha bao la kuongoza la Prisons, katika mchezo wa sare ya bao 1-1 uliopigwa kwenye uwanja wa Mkapa.
Akizungumzia mipango yao kuelekea mchezo dhidi ya Al Merrikh Gomes amesema: “Hatukufurahishwa na matokeo ya mchezo wetu uliopita dhidi ya Prisons, lakini tumechukua hiyo kama changamoto hivyo tumejipanga kuhakikisha tunarejea tukiwa bora kwenye mchezo ujao dhidi ya Al Merrikh.
“Naamini vijana wangu watakuwa na wakati mzuri dhidi ya Al Merrikh, na ni lazima tucheze katika levo ambayo tulicheza dhidi ya Al Ahly na As Vita,”