Dereva, gari lililomteka Mo Dewji latambulika

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amesema jeshi hilo limefanikiwa kutambua aina ya gari ambalo limetajwa kumteka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji pamoja na dereva aliyekuwa akiendesha gari hiyo aina ya Surf.
Mkuu wa jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, jeshi hilo kupitia vyombo vya uchunguzi vilifanikiwa kukamata ganda la risasi yenye urefu wa milimita 9 ambazo ilitumika wakati wa tukio la kupotea kwa Mohamed Dewji.
Kamanda Sirro amesema gari hilo limesajiliwa kwa namba za usajili za kutoka nchi jirani ambapo inaelezwa gari hilo lilifanikiwa kuingia mwanzoni mwa mwezi septemba mwaka huu.
CCTV camera zimetusaidia zimeweza kutambua gari baada ya kufanya uchunguzi tumefanikiwa kulijua gari na tumezungukia maeneo yote ambayo hilo gari lilipita na bado watu wetu wameendelea kufatilia kama gari lilielekea maeneo ya Silver sand au Kawe.”
Ila tumepata taarifa kwamba gari hilo limetokea nchi jirani, na watu wetu wamekwenda mpakani na wameona gari hii likipita mpakani tarehe moja septemba. Nani alikuwa dereva wa ile gari imefahamika, nani alikuwa dereva wa ile gari na watu wetu interpool wanalifanyia kazi.”
 
Aidha IGP Sirro amewataka watu wenye uwezo wa kifedha nchini kujiwekea ulinzi wa kutosha kwa ajili ya usalama wa maisha yao.
IGP Sirro akionesha gari lililofanya utekaji wa Mo Dewji
IGP Sirro akionesha gari lililohusika katika tukio la utekaji wa Mo Dewji

Tukio la kutekwa Mo Dewji lilivyotokea;

Mfanyabiashara huyo alidaiwa kutekwa Alhamisi ya wiki iliyopita wakati alipokwenda kufanya mazoezi katika hoteli ya Collessium iliyopo Oysterbay jijini Dar es salaam.
Siku iliyofuata jeshi la polisi lilianza kuwakamata watu mbalimbali kwa mahohiano maalumu akiwemo Afisa Habari wa Simba, Haji Manara aliyedaiwa kusambaza taarifa hizo katika mitandao ya kijamii, taarifa ambayo polisi imedai hazikuwa na ukweli wowote.

Watu waliokamatwa;

Jumla ya watu 26 walikamatwa kupitia tukio hilo, ambapo 19 kati yao waliachiwa huru kwa dhamana akiwemo Haji Manara, huku kukiwa hakuna taarifa yoyote ya kuachiwa huru kwa wengine saba waliobakia mpaka sasa.
Viongozi wa siasa wanavyomlilia;
Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini wameandika na kuzungumza ujumbe mbalimbali wakionesha kusikitishwa na tukio hilo, akiwemo Zitto Kabwe (ACT-wazalendo), Hussein Bashe (CCM), Nape Nnauye (CCM), Godbless Lema (CHADEMA), Ismail Jussa (CUF). 
Inaaminika kuwa Mo Dewji, kupitia uwekezaji wa makampuni yake nchini amefanikiwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya elfu 25, huku akichangia asilimia takribani 3.1 kwenye uchumi wa taifa.

Source: EATV TZ

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post