Jeshi
la Iran (IRGC) limerusha makombora ya balestiki na kupiga kambi za
kijeshi za Marekani nchini Iraq, kama jibu la kuuawa Jenerali Qassem
Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha SEPAH.
Taarifa ya IRGC imesema kuwa, Iran imetoa jibu hilo
kwa Marekani alfajiri ya leo, ambapo imelenga uwanja wa ndege wa
kijeshi wa Marekani wa Ain al-Assad katika mkoa wa al-Anbar, magharibi
mwa Iraq.
Jeshi la Iran limeitaka Marekani
iwaondoea wanajeshi wake wote katika nchi hiyo ya Kiarabu, likisisitiza
kuwa halitatenganisha kati ya Marekani na Israel katika kujibu mapigo ya
kuuawa Jenerali wao.
Waziri wa Mambo ya Nje
wa Iran, Mohammad javad Zarif amezungumzia kuhusu jibu hilo la Iran
katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuandika:
"Iran imechukua hatua madhubuti ya kujihami kwa mujibu wa Sura ya 51 ya
Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa kulenga kambi ya jeshi ambayo ilitumiwa
katika shambulizi la kioga dhidi ya raia na maafisa wetu wa ngazi za
juu. Hatutaki kukuza mambo wala vita, lakini tutajihami dhidi ya uvamizi
wowote."
Wizara ya Ulinzi ya Marekani
(Pentagon) imethibitisha habari hizo za kuvurumishwa makumi ya makombora
ya balestiki kuelekea katika kambi ya jeshi la Marekani nchini Iraq.
Tags
Kimataifa
