MSHAMB-ULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Amissi Tambwe raia wa Burundi 
ameibuka na kuweka wazi kwamba katika kipindi hiki cha usajili hana 
mpango wowote wa kuondoka ndani ya timu hiyo kutokana na kujiona ana 
deni la kulilipa baada ya kushindwa kuonyesha makali msimu uliopita.
Mshambuliaji huyo hakuwa na msimu mzuri katika msimu uliomalizika hivi 
karibuni baada ya kuandamwa na majeraha ya kila mara ya goti ambayo 
yalimsababisha kumaliza ligi akiwa hajafunga bao lolote lile.
Akizungumzia juu ya mustakabali wake ndani ya kikosi hicho, Tambwe 
ambaye yupo kwao kwa ajili ya mapumziko baada ya ligi kumalizika 
mshambuliaji huyo amesema hawezi kuondoka katika timu hiyo kwa sasa 
kufuatia kuvumiliwa kwa msimu mzima huku akiwa na majeraha ya mara kwa 
mara ambapo anataka kulipa fadhila kwenye msimu ujao.
“Kwa msimu uliopita sikuwa na kiwango kikubwa hivyo ninajiona kwamba 
nina deni la kulipa kwa Yanga ambao wamenivumilia licha ya kwamba 
nilikuwa na majeraha, ninachofanya sasa ni kujiandaa kwa ajili ya msimu 
ujao niwe vizuri,” alisema mshambuliaji huyo.
