Nyota wa Klabu ya Yanga na wawakilishi pekee Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa, Thaban Kamusoko amefunguka na kudai sababu kubwa iliyowasababisha kufanya vibaya katika michezo yao Ligi ni kutokana na kubanwa na ratiba japo ambalo lilipelekea kushindwa kupata muda mzuri wa kujiandaa.
Kamusoko ametoa kauli hiyo jioni ya leo Mei 22, 2018 muda mchache ilipomaliza mechi yao dhidi ya Mbao FC ambapo Yanga imefanikiwa kutoka na ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa na mchezaji huyo na kuifanya timu yake kupata matokeo mazuri baada ya kupitia msoto mkali wa vipigo vitano na sare nne kwenye mechi zilizopita katika mashindano yote ya ligi kuu.
"Cha kwanza namshukuru Mungu tumepata ushindi, katika mchezo wa leo kitu ambacho tulikuwa tumejiwekea akilini ni kupata ushindi kwasababu Yanga ukiangalia ni timu kubwa yenye watu wengi kwa hiyo inahitaji ushindi kwa kila mechi", amesema Kamusoko.
Aidha, Kamusoko amesema sababu kubwa ya Yanga kufanya vibaya katika michezo yake ya hivi karibuni ni kutokana na kubanwa na ratiba ambayo iliwapelekea kushindwa kupumzika vizuri ili wapate kujiandaa na michezo iliyokuwa inawakabiri.
Pamoja na hayo, Kamusoko amesema watajitahidi kufanya vizuri katika michezo yao miwili iliyosalia ili waweze kujikunyakulia alama 6 ambazo zitawaweza kuwaweka sehemu nzuri kwenye msimamo wa ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa ushindi wa leo, Yanga imeweza kufikisha alama 51 kwenye mechi 29 na kuendelea kuwa katika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye alama 55 na Simba yenye alama 68 kileleni.
Tags
Michezo