HOFU YA ZIDANE DHIDI YA LIVERPOOL YAPANDA





Katika kuelekea mchezo wa fainali wa mashindano ya klabu bingwa Ulaya, kocha mkuu wa timu ya Real Madrid Zinedine Zidane amesema kitu pekee anachohofia katika mchezo huo ni washambuliaji wa Liverpool wakiongozwa na Mohamed Salah.


Kwa mujibu wa gazeti la Independent, Zidane amesema hayo leo Mei 22, 2018 wakati akiongea na waandishi wa habari na kuongeza kuwa Liverpool ni timu bora baada ya kuwa na msimu mzuri katika ligi kuu ya England na pamoja michuano ya Ulaya na timu hiyo inayostahili kuwepo katika fainali ya klabu bingwa Ulaya.

“Ninachoogopa kuhusu hii timu (Liverpool), kinachozungumziwa ni wachezaji  watatu wa mbele au mapungufu ya safu ya ulinzi, wanastahili kuwepo katika fainali kama sisi, ni wachezaji wenye ukaribu sana, jukumu letu pamoja na benchi la ufundi ni kuhakikisha tunajiandaa vya kutosha na mchezo huo kujua mapungufu ya mpinzani wetu na kuwaadhibu” amesema Zidane.

Zidane ameongeza kuwa ikitokea amepoteza mchezo huo bado haitakuwa kama ni kushindwa bali jambo pekee aliloshindwa katika msimu huu ni kutolewa katika hatua ya Robo fainali dhidi ya Leganes katika kombe la mfalme “Copa del Rey” nchini Hispania.

Jumamosi Mei 26, 2018 mabingwa watetezi Real Madrid ya Hispania watakabiliana na klabu ya Liverpool kutoka England katika  mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa Ulaya katika Mji wa Kiev nchini Ukraine.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post