Mwakyembe Awaonya Watumiaji wa Mitandao ya Kijamii


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa faida yao binafsi na sio kupeleka uchafu ambao umezuiwa na sheria zingine. 

Dkt. Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo Aprili 17 Bungeni jijini Dodoma kwenye kikao cha 11 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mbunge Goodluck Mlinga alipoihoji serikali kuwa ina mpango gani wa kuwadhibiti watumiaji wa mitandao ya kijamii hususani 'instagram' kutokana kumekuwepo na vikundi vya 'timu Wema', 'timu Zari' na 'timu Shilole' n.k kuwa wanatoa lugha chafu za kutukana watu jambo ambalo linachangia upotoshaji wa maadili na utamaduni wa kitanzania. 

"Tulitunga sheria ya EPOCA mwaka 2010 ilikosa kanuni za kubana maudhui hasa upande wa mitandao. Sasa tunazo hizo kanuni na zimeshaanza kufanya kazi. Naomba nitoe wito kwa vijana wote nchini, mitandao sio kokolo ya kupeleka uchafu wote ambao umezuiliwa na sheria zingine, hii nchi ina tamaduni zake. Tunahitaji kulinda kizazi cha leo, kesho na kesho kutwa cha taifa hili", amesema Dkt. Mwakyembe. 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amesema changamoto kubwa inayoikabili taifa la Tanzania ni athari ya utamaduni wa nje kwa maadili mila na desturi kupitia muingiliano mkubwa wa watu wa dunia kwa njia ya utalii, biashara n.k.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post