Maafa ya Mvua: RC Makonda Ataka Mamlaka Husika Kufunga Shule


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameziomba mamlaka za elimu kufunga shule kwa siku mbili kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. 

Makonda amesema hayo leo Jumatatu, Aprili 16 alipokuwa akitembelea maeneo mbalimbali yaliyoathirika na mvua zinazoendelea kunyesha  kwa siku tatu mfululizo jijini Dar es Salaam. 

Amesema mvua zikinyesha miundombinu inaharibika ikiwamo barabara na shule, hivyo wanafunzi wabaki majumbani hadi hali itakapotengemaa. 

“Nimeziomba mamlaka za elimu kufunga shule kwa siku mbili, hadi tutakapowaambia siku ya Jumatano kulingana na hali itakavyokuwa kuwa, kwa sababu mvua zinaendelea kunyesha maeneo mengi yamejaa maji kwa watoto hili siyo salama sana,” amesema Makonda. 

Makonda amefafanua kuwa hadi sasa watu waliofariki mkoani Dar es Salaam kutokana na mvua hizo ni zaidi ya saba. 

“Bado tunaendelea kupokea taarifa, lakini hadi sasa wamekufa watu saba hadi 10, madhara ni makubwa tunawaomba wananchi watulie majumbani mwao hadi hapo hali itakapokuwa shwari.” 

Amesema hakuna sababu ya wananchi kusubiri kuondolewa na polisi wala kugombana na Serikali wanapoambiwa wahame katika maeneo hatarishi ikiwamo mabondeni. 

Makonda amesema wamekuwa wakitoa tahadhari mara kadhaa na kuainisha sababu zinazowataka kuhama katika maeneo hayo mojawapo ikiwa ni mafuriko. 

“Tunaendelea kukusanya taarifa, lakini barabara nyingi zimeharibika, nyingine zimejaa maji, kwa wanaoishi maeneo hatarishi wachukue tahadhari mapema hali ni mbaya,” amesema Makonda.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post