Polisi nchini Iran wamekamata wanawake 29 kwa tuhuma za kushiriki maandamano ya kupinga sheria ambayo inasema kuvaa hijab kwa wanawake kuwa ni jambo la lazima nchini humo.
Inaelezwa kuwa suala la wanawake kubanwa kisheria kuvaa hijab ni agenda ambayo imekuwa ikizungumzwa kwa takribani miaka 40 na kwa sasa wanawake nchini humo wameanza kupinga suala hilo kwa migomo na maandamano.
Mwandishi wa Habari anayeishi Marekani na Mwanaharakati Masih Alinejad alianzisha Kampeni inayojulikana kama ‘White Wednesdays’ yaani Jumatano Nyeupe mnamo May 2017 ambayo inashawishi wanawake kuvaa hijab za rangi nyeupe au kuzivua kabisa ili kupinga sheria hiyo.
Masih ameviambia vyombo vya habari kuwa polisi nchini Iran mwaka 2014 walitangaza kuwaonya, kuwatia mbaroni au kuwapeleka mahakamani wanawake Milioni 3.6 kwa kuvaa hijab ‘mbaya’ hivyo kukamatwa wanawake hao kipindi hiki sio suala geni.