Dansa wa kundi la Wasafi Classic (WCB), Mose Iyobo amesema hajawashambulia watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds kama ilivyoelezwa.
Amesema madai ya kuwashambulia watangazaji hao na wafanyakazi wengine wa televisheni hiyo ameyasikia kwenye mitandao ya kijamii na katika kipindi hicho jana, Februari 2, 2018.
“Nimesikia kupitia kipindi chao na kwenye mitandao ya kijamii, sina nguvu hiyo, mimi si baunsa wala mkorofi wa kufikia hatua hiyo, ” amesema Iyobo alipozungumza na MCL Digital leo Februari 3, 2018.
Amedai wanahabari hao walifika dukani kwake maeneo ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam na alipobaini lengo la ujio wao aliondoka.
“Sikuwapiga, nilipobaini wamekuja kwa lengo la kutengeneza habari zao wanazorusha kwenye kipindi cha Shilawadu, sikufurahishwa na hilo nikaondoka zangu,”amesema.
“Nilijua tayari wana habari vichwani mwao na walikuja pale kwa lengo la kukamilisha walichonacho na siyo kusikia kutoka kwangu, wakati mwingine hizi habari huwa na madhara katika jamii na familia zinazotuzunguka. Nikaamua kujiepusha kwa kuondoka eneo hilo, sikuwapiga na sina jeuri hiyo.”
Akizungumzia tuhuma hizo mmoja wa viongozi wa WCB, Babu Tale amesema wamemuachia suala hilo Iyobo kwa kuwa ni mambo binafsi na hakuna mahali popote yalipotajwa kuhusiana na kazi zake.
“Ingekuwa habari hiyo inahusiana na kazi tungezungumzia, hayo ni mambo binafsi sisi hatuwezi kuingilia,” amesema.
Jana Februari 2, 2018 watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kupitia mitandao ya kijamii na kipindi hicho walieleza kushambuliwa na Iyobo ambaye ni mpenzi wa mwigizaji Aunt Ezekiel.
Mbali na kushambuliwa wamesema Iyobo aliharibu vifaa vya kutayarishia kipindi hicho, “Usiku wa leo wakati tukiwa kazini tumenusurika kumwagwa damu na mtu tuliyemfuata kumuomba mahojiano, kati yetu kuna walioumia viuno na mikono, pia kuna uharibifu wa vifaa vyetu vya kazi.”
Wanahabari hao wakati wakitangaza kipindi hicho walikuwa wamejifunga bandeji mikononi, huku mmoja akiwa amesimama kwa msaada wa gongo, shingoni akiwa amevaa kifaa maalumu.