Mashinji: Mgombea Wetu wa Udiwani Alitekwa Alilazishwa Kupokea Milioni 8 Ili Ajitoe

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Buhangaza Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Athanas Makoti (28) alilazimishwa kupokea rushwa ya Sh8milioni na watu waliomteka na kumjeruhi ili ajitoe kwenye uchaguzi.
Mashinji: Mgombea Wetu wa Udiwani Alitekwa Alilazishwa Kupokea Milioni 8 Ili Ajitoe


Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 7, 2018 makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Dk Mashinji ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuchukua hatua.

Makoti alitekwa Februari 2, 2018 katika mazingira ya kutatanisha na kupatikana Februari 5, 2018 saa moja asubuhi akiwa ametelekezwa na watu wasiojulikana jirani na Hospitali ya Kagando iliyopo Wilaya ya Muleba. Mgombea huyo amelazwa katika hospitali hiyo mpaka sasa.

Dk Mashinji amesema Makoti alikuwa anatoka kwenye maandalizi ya uchaguzi, akaita bodaboda ili arejee nyumbani lakini likatokea gari nyuma yake na kumchukua kwa nguvu.

“Watekaji hao walimfunga kitambaa usoni akapoteza fahamu. Walimzungusha maeneo mbalimbali na alipozinduka hakujua aliko. Walimtaka akubali kupokea Sh8 milioni na ajitoe kwenye uchaguzi, hata hivyo alikataa ndipo wakaanza kumtesa,” amesema Dk Mashinji,

“Hizi ni njama za kisiasa kutaka kuvuruga uchaguzi katika kata ya Buhangaza,” amesema.

Amesema kwa mujibu wa maelezo ya mgombea huyo, alitekwa kwa madhumuni ya kisiasa.

“Tunalaani  kitendo cha mgombea wetu kutekwa, kuteswa na kulazimishwa kupokea fedha ili ajitoe kwenye uchaguzi,” amesema.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post