Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amefikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya leo Januari 22, 2018 kusikiliza kesi inayomkabili ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Sugu pamoja Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga walifikishwa mahakamani hapo Januari 19, 2018 lakini mahakama ilizuia dhamana zao na kuwarejesha rumande hadi leo.
Siku hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite alitoa uamuzi wa kuwarejesha rumande, kwamba kesi hiyo inatakiwa isikilizwe mfululizo kwa muda mfupi na washtakiwa wakiwa wanafika mahakamani hapo wakitokea mahabusu.
“Mahakama hii inataka kusikiliza kesi hii kwa muda mfupi sana, ndani ya wiki moja kuanzia Jumatatu ijayo (leo) iwe imeamuriwa, hivyo washtakiwa wataendelea kuwekwa mahabusu,” amesema Mteite.
Sugu na Masonga wameshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo waliyatoa katika mkutano wa hadhara walioufanya Desemba30 mwaka jana wakiwa viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya