Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeiomba Serikali kuondoa mabadiliko ya Sheria ya Ardhi yaliyomo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ili kuepuka madhara ya kiuchumi yanayoweza kusababishwa na mabadiliko hayo iwapo yatapitishwa.
Katika kuhimiza hilo, TPSF imemuandikia barua Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ikimtaka kuwashirikisha wadau kabla ya muswada huo kujadiliwa na Kamati ya Bunge.
Msimamo wa TPSF unafanana na wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambacho kimesema iwapo marekebisho hayo yatapitishwa na sheria kuanza kutumika, yataathiri mfumo wa rehani nchini.
Mjumbe wa Kamati ya Katiba na sheria ya TLS, John Seka alisema kwa muda mrefu wananchi wengi wamekuwa wakitumia mashamba kama rehani kwenye taasisi za fedha.
Alisema wamewasilisha maoni yao Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria inaouchambua muswada huo unaomtaka mmiliki wa shamba ambalo halijaendelezwa au kuendelezwa kidogo, kutumia fedha anayokopa kuliendeleza zaidi.
Jana, mkurugenzi mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema muswada huo unapaswa kuondolewa kabisa bungeni kwani endapo kosa lolote litafanyika, madhara yake ni makubwa kwenye uchumi.
“Inawezekana Serikali ina lengo zuri, lakini hatukushirikishwa. Uwekezaji utakufa nchini kwa sababu wengi hukopa ili kuendeleza biashara walizonazo jambo linalozuiwa kwa sasa,” alisema Simbeye.
Kwa hali hiyo, alisema sekta ya kwanza kuanguka itakuwa ya benki na taasisi za fedha ambazo zitakosa wateja.
TPSF imeipongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha mazingira ya biashara hasa kwa kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kuwekeza, lakini imetoa angalizo kwa marekebisho yanayopendekezwa.
TPSF imepokea malalamiko kutoka kwa wanachama, benki na taasisi za fedha, wamiliki wa viwanda pamoja na wakulima kuhusu mabadiliko yanayopendekezwa, inasema barua hiyo.
Miongoni mwa hoja zilitolewa na taasisi hiyo ni kutoshirikishwa kwa wadau katika utungaji wa mabadiliko hayo ili wawasilishe maoni yao.
Imesema kwa namna muswada huo ulivyoandaliwa, Serikali inaweza isipate mafanikio inayoyatarajia na mapendekezo ya vifungu hivyo vitatu yanaweza kuwa na athari kwa uchumi wa nchi.
“Kwa barua hii, tunaiomba wizara yako iuondoe mara moja muswada huo kabla haujajadiliwa na Kamati ya Bunge au Bunge lenyewe mpaka wadau, ikiwamo TPSF watakaposhirikishwa,” inasema barua hiyo.
Muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria tano ambazo ni Sura ya 25 ya Sheria ya Ufilisi, Sura ya 439 ya Sheria ya Bajeti, Sura ya 113 ya Sheria ya Ardhi na Sura ya 238 ya Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuondoa mapungufu mbalimbali yaliyomo katika utekelezaji wa sheria hizo.
Marekebisho ya Sheria ya Ardhi ambayo TPSF inapendekeza maoni yao yazingatiwe, inabadili masharti yaliyopo kwenye Kifungu cha 45 kwa kuongeza adhabu ya ukiukwaji wa masharti kwa mtu anayeweka dhamana ya miliki ya ardhi.
Kwenye sheria inayofanyiwa marekebisho, vifungu vya 120A, 120 B na 120 C vimeongezwa kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mkopo uliotolewa kwa dhamana ya miliki ya ardhi Tanzania zitumike kuendeleza sehemu ya ardhi iliyowekwa rehani kwa miliki zote ambazo hazijaendelezwa.
Marekebisho hayo yanawataka wote wawili; mkopaji na mkopeshaji, kuwasilisha taarifa kwa kamishna wa ardhi. Licha ya hilo, yanataka fedha itakayopatikana iwekezwe Tanzania.
Aidha, muswada unataka benki na taasisi zote za fedha zinazotoa mkopo husika; ndani na nje ya nchi kuwasilisha tamko kwa kamishna wa ardhi kwamba fedha hizo zitawekezwa Tanzania.
Maana yake, mkopo wa fedha zozote zitakazokopwa kwa dhamana ya ardhi ya Tanzania kisha zikawekezwa nje, utakuwa batili.
Waziri Lukuvi amewataka wadau wenye maoni kuhusu marekebisho yanayopendekezwa kwenye muswada huo kuyawasilisha kwenye kamati husika ya Bunge.
“Huo ndio utaratibu. Kama kuna malalamiko yoyote, ni vizuri yawahishwe wakati huu vikao vinapoendelea, yatachambuliwa,” alisema