Waziri wa ulinzi nchini Kenya, mkuu wa polisi pamoja na afisa mkuu kutoka idara ya uhamiaji wameagizwa kufika mahakamani hii leo.
Hatua hii imekuja baada ya serikali kukaidi maagizo yaliyotolewa na mahakama juu ya kumwachilia huru wakili wa upinzani Miguna Miguna na kumfikisha hadi mahakamani asubuhi ya leo.
Hii ni siku ya pili kwa Miguna kukesha katika uwanja ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, tangu wakili huyo alipowasili nchini Kenya kutoka Canada siku ya Jumatatu.
Bw Miguna Miguna alijaribu kurejea Kenya Jumatatu lakini akazuiwa kuingia baada yake kudaiwa kutowasilisha hati ya kusafiria ya Canada ambayo ilitumiwa kumsafirisha kwa nguvu hadi Canada.
Wakili huyo alisisitiza kwamba ni raia wa Kenya na hafai kuzuiwa kurejea.
Mwandishi wa BBC, Victor Kenani amesema ,umati wa watu walijaza chumba cha mahakama cha Mlimani mjini Nariobi, wakisubiri Miguna kuletwa mbele ya mahakama lakini hakutokea,
Mawakili wa serikali wakisema kuwa hawakuweza kumleta sababu ya mchakato mrefu uliokuwepo.
Upande wa pili mawakili wa Miguna walisema serikali imekaidi moja kwa moja agizo la mahakama na hatua kali ilitakiwa kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa serikali.
Jaji George Odunga alikana hoja za mawakili wa serikali na kusema mahakama lazima iheshimiwe na Miguna aletwe makahamani.
Wakati huo huo, kumekuwa na maandamano katika mji wa Kisumu, magharibi mwa Kenya ambapo wa wanaandamanaji wamechoma magurudumu na kuzuia barabara.
Miguna alitimuliwa kwenda nchini Canada mwezi Februari baada ya kuonekana kuidhinisha kiapo cha Bw Raila Odinga alipokuwa anajiapisha kuwa 'Rais wa Wananchi' mwezi Januari.
Tags
Afrika