Ujerumani walishindwa kwa mara ya kwanza katika mechi 23 baada ya mshambuliaji wa Manchester City Gabriel Jesus kuwafungia Brazil bao moja na kuwapa ushindi wa 1-0 jijini Berlin.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mataifa hayo mawili kukutana uwanjani tangu Ujerumani walipowaaibisha Brazil 7-1 katika nusufainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 mjini Belo Horizonte.
Jesus aliwaweka Brazilmbele kwa mpira wa kichwa dakika za mwishi mwisho kipindi cha kwanza, dakika ya 37.
Alikuwa amepoteza nafasi nyingine ya kufunga muda mfupi awali na kipindi cha pili alipoteza nafasi nyingine pia ambapo aliumpiga mpira nje kwa kichwa lango likiwa wazi baada ya Trapp kutokea kujaribu kuudaka mpira kona ilipopigwa.
Mjerumani Julian Draxler apia alipoteza nafasi ya kufunga mechi ikikaribia kumalizika.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Ujerumani ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia na walioorodheshwa nambari moja duniani kushindwa tangu walipolazwa na Ufaransa nusufainali Euro 2016.
Tangu wakati huo, vijana hao wa Joachim Low walikuwa wameshinda mechi 16 na kutoka sare mechi sita kabla ya mechi hiyo iliyochezewa uwanja wa Olympiastadion.
Brazil kulipiza kiasi
Ingawa ilikuwa mechi ya kirafiki, ushindi huo ni wa maana sana kwa Brazil ambao wameandamwa na kushindwa kwao Kombe la Dunia miaka minne iliyopita nchini mwao.
- Mourinho: Mwenye akili zake anaielewa hali ya Manchester United
- Jedwali la Msimamo wa ligi ya EPL 2017/18
Kabla ya mechi, mkufunzi wao Tite aliyepewa kazi mwaka 2016 alikuwa amesema: "Hii ina maana kubwa sana kisaikolojia - hakuna anayehitaji kujidanganya kuhusu hilo," Titea aliambia jarida la Kicker.
"Matokeo hayo ya 7-1 ni kama mizimu, watu bado huyazungumzia. Kadiri unavyoyazungumzia zaidi, ndivyo mizimu hii inavyochukua muda mrefu kutoweka."
"Nilikuwa ninatazama mechi hiyo (ya mwaka 2014) niliwa nyumbani Sao Paulo na mke wangu na baada ya bao la tatu kufungwa, alianza kulia," amesema Tite.
"Hili lilinigusa sana, nami nikaanza. Ulikuwa wakati mzuri sana kwa Ujerumani, kila kombora lililolenga goli lilikuwa bao - mambo kama hayo huwa hayatokei hata kwenye michezo ya video ya kompyuta."
Tite alitilia mkazo maneno yake kwa kuweka uwanjani kikosi imara zaidi, ambapo mchezaji pekee aliyemkosa ni Neymar ambaye anauguza jeraha. Ujerumani kwa upande wao walibadilisha wachezaji sita kwenye kikosi kilichotoka sare 1-1 na Uhispania Ijumaa na waliwabadilisha wachezaji watano mechi ikiendelea tofauti na Brazil ambao waliingia nguvu mpya mmoja pekee.
Wageni Brazil walijiweka kifua mbele dakika ya 37 kwa mpira wa kichwa wa Jesus ambao kipa nambari tatu wa Ujerumani Kevin Trapp hakuuweza kuunasa.
Wachezaji wawili nyota wa Manchester City Leroy Sane na Ilkay Gundogan walishindwa kuifaa Ujerumani na wote waliondolewa uwanjani kabla ya mechi kumalizika.
Ujerumani walipata kombora la kulenga goli dakika ya 92 lakini kipa wa Brazil Alisson akatema nje mpira huo kutoka kwa Draxler.
Brazil waliwalaza Ujerumani katika fainali ya Michezo ya Olimpiki 2016 - michezo ambayo haikushirikisha kikosi kamili cha taifa - lakini hii ilikuwa mara ya kwanza kwa timu za taifa za mataifa hayo mawili kukutana.
Ushindi huo utawasaidia kuponya makovu ya miaka minne iliyopita.
Argentina wafungwa 6-1
Kwingineko mjini Madrid, Isco alifunga mabao matatu na kuwasaidia Uhispania kupata ushindi mnono wa 6-1 dhidi ya Argentina ambao walifika fainali Kombe la Dunia 2014.
Uhispania waliongoza 2-0 baada ya Diego Costa kumbwaga Sergio Romero kisha Isco akafunga bao lake la kwanza.
Argentina, waliomkosa Lionel Messi ambaye anauguza jeraha, walikomboa moja kupitia ulled Nicolas Otamendi aliyefunga kwa kichwa na kufanya mambo kuwa 2-1.
Isco na Thiago Alcantara kisha walifunga na kufanya mambo 4-1 kabla ya nguvu mpya Iago Aspas kuongeza la tano.
Isco alikamilisha ushindi wao wa kufunga bao la kukamilisha 'hat-trick' yake.
Uhispania ambao walishinda Kombe la Dunia 2010 sasa hawajashindwa mechi 18 tangu Julen Lopetegui alipochukua usukani baada yao kuondolewa mapema hatua ya muondoano Euro 2016.
Pogba awafungia Ufaransa
Paul Pogba naye alifunga kupitia mkwaju wa adhabu naye Kylian Mbappe akafunga mawili na kuwawezesha Ufaransa kulaza wenyeji wa Kombe la Dunia Urusi 3-1 mjini St Petersburg.
Didier Deschamps alifanya mabadiliko saba kwenye kikosi kilichoshindwa na Colombia 3-2 Ijumaa, ambapo Pogba alirejeshwa kikosini kutoka kwenye benchi.
Fedor Smolov aliwafungia wenyeji bao la kufutia machozi.
Panama waona moto Uswizi
Panama, ambao wamepangwa kundi moja na England katika Kombe la Dunia, nao walicharazwa vikali na Uswizi mechi ya kirafiki baada ya kubebeshwa magoli sita bila jibu.
Mabao yote yalifungwa na wachezaji tofauti.
Panama wanajiandaa kushiriki Kombe la Dunia mara ya kwanza.
Blerim Dzemaili, Granit Xhaka, Breel Embolo na Steven Zuber waliwapa Waswizi uongozi wa 4-0 kabla ya mapumziko.
Wachezaji Josip Drmic na Fabian Frei waliotoka benchi walifunga mengine mawili kipindi cha pili na kukamilisha ushindi Lucerne.
Uswizi wamepangwa na Brazil, Costa Rica na Serbia Kundi E.
Panama - ambao wameshindwa mechi tatu na kutoka sare mechi moja - dhidi ya Wales - mechi nne za karibuni za kirafiki walizocheza, wamepangwa kucheza na England mechi ya pili ya Kundi G mnamo 24 Juni mjini Nizhny Novgorod.
England walitoka sare 1-1 na Italia uwanjani Wembley.
Jamie Vardy alifungia vijana hao wa Gareth Southgate dakika ya 26 alipombwaga kipa Gianluigi Donnarumma baada ya mkwaju wa adhabu uliopigwa haraka na Jesse Lingard kuwapata Italia wakiwa hawajajiandaa vyema.
Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Vardy akichezea England baada ya siku 366.
Italia walisawazisha dakika ya 87 kupitia mkwaju wa penalti baada ya teknolojia ya msaidizi wa refa kuonesha James Tarkowski alikuwa amemkanyaga Federico Chiesa mguuni.
Lorenzo Insigne alimbwaga kipa Jack Butland mechi ikiwa imesalia dakika tatu.
Tags
MICHEZO KIMATAIFA