Wadau wa usafirishaji wameunga mkono kauli ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ya namna askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki) wanavyotakiwa kufanya kazi na wametaka isambae kwa makamanda wa mikoa mingine.
Juzi, Kamanda Mambosasa alizungumzia jinsi trafiki anavyotakiwa kufanya kazi iwapo atasimamisha gari, makosa anayotakiwa kuhoji na faini zinazopaswa kutozwa kulingana na wakati.
Pia alieleza kuwa polisi wanaozunguka na pikipiki maarufu kwa jina la tigo hawaruhusiwi kutoza faini baada ya kukamata gari.
Mambosasa alisema si kila kosa linapaswa kutozwa faini na kushangazwa na askari wanaokamata magari mchana kwa kosa la kutokuwa na taa.
Akitoa maoni yake kuhusu kauli ya Mambosasa, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu alisema imekuja wakati muafaka na wanaiunga mkono kwa asilimia 100 kutokana na hali halisi iliyopo barabarani kwa sasa.
Alisema imefikia hatua wamekuwa waoga hata kufanya kazi yao ya usafirishaji abiria kutokana na kero za askari wa usalama barabarani hasa katika kutafuta makosa na kutoza faini.
“Nimemuelewa Mambosasa na ninamuunga mkono kwa sababu huko njiani faini zimekuwa nyingi mno, unapotoka Ubungo unakaguliwa na kuruhusiwa, hii peke yake ingetosha kuonyesha gari lipo salama lakini kila sehemu kuna ukaguzi na faini nyingi,” alisema.
Alisema kwa kuwa Mambosasa ameongea akiwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ipo haja kwa makamanda wa mikoa mingine, kusimamia ukweli huo na kuondoa vikwazo kwa madereva barabarani.
“Ujumbe wa Mambosasa uwe ujumbe wa nchi nzima ili kila mkoa askari wa usalama barabarani na madereva kila mtu ajue wajibu na haki yake akiwa barabarani,” alisema.
Alisema hakutakuwa na maana kama askari wa usalama wa barabarani wa Dar es Salaam watafuata sheria ikiwamo kutosimamisha gari bila kujua kosa la msingi kama mikoa mingine haitafanya hivyo.
Mrutu alisema kuna wakati basi linaweza kupasuka kioo njiani wakati wa safari lakini wakikutana na trafiki hata kama watamweleza uhalisia bado watatozwa faini jambo ambalo sio sawa
“Sasa upo barabarani kioo kimepata ‘crack’ (ufa) utapeleka wapi ukutane na fundi? Si mpaka umalize safari? Nadhani wajifunze pia kutoa onyo kwa makosa mengine na sio kila kosa ni faini,” alisisitiza.
Katibu wa Umoja wa Usafirishaji Abiria Dar es Salaam (Uwadaa), Selemani Kimowe alisema kauli ya Mambosasa ilipaswa kuzungumzwa na viongozi wengine wa polisi kwenye mikoa yote.
Alisema kero kubwa wanayopata kutoka kwa askari barabarani ni wingi wa faini baadhi zikiwa hazina ulazima na kutaka kuwepo muafaka baina ya askari, madereva na wadau wengine wa usafirishaji.
Alisema kuna wakati hutozwa faini hadi Sh700,000 kwa wiki na wapo ambao wanadaiwa mpaka Sh10 milioni wakati si kila kosa linapaswa kutozwa, kama alivyosema Kamanda Mambosasa.
“Wakati mwingine ndio hivyo makosa ya kutafuta japo Mambosasa ameelezea nadhani kinachotakiwa ni ushirikiano baina yetu, tusikomoane kwa sababu sote lengo letu ni kusafirisha abiria kwa usalama,” alisema.
Alisema kauli ya Mambosasa haitakuwa na maana kama askari hawatajua sheria na makosa gani yanapaswa kutozwa faini na kwa wakati gani.
Kimowe alisema kinachofanyika wakati wa safari ni kwamba kosa la dereva huandikiwa mmiliki wa gari jambo ambalo alisema sio sawa.
Alisema kwa sababu lengo hasa ni kusafirisha abiria kwa usalama, linapotokea kosa, mmiliki wa gari husika anapaswa kupewa taarifa achukue hatua ikiwa ni pamoja na kulipa faini kabla deni halijawa kubwa na dereva kuchukuliwa hatua.
“Kuna wakati askari anaweza kuingiza kosa bila kutoa taarifa na hii inatokea kwa sababu kila siku wanawaona madereva, wanazo leseni zao na namba za magari. Haya yote hayapaswi kufanywa kama Mambosasa alivyosema lakini huwa tunalipa tu,” alisema.
Alisema kuna wakati waliamua kwenda kwa viongozi wa juu kabisa wa jeshi la polisi kutokana na faini kuwa kubwa. Mjumbe wa umoja wa madereva wa mabasi, Hussein Ally alisema kuna haja ya kutoa elimu kwa pande zote mbili kujua wajibu na haki badala ya upande mmoja usio na nguvu kuendelea kuonewa.
“Unaweza kujiamini kuwa huna kosa, askari akikusimamisha akatafuta hadi akalikuta na kuandika faini hii haijakaa sawa kabisa, Mambosasa akae na askari wake awaelekeze,” alisema.
Alisema kinachotakiwa kufanywa ni kwa wadau wote kushirikiana bila kukomoana kama inavyofanywa hivi sasa.