Muigizaji wa muda mrefu nchini, Mahsein Awadh maarufu kama Dk Cheni, amefunguka kuhusu tetesi zilizozagaa mitandaoni, zikimhusisha kuhusu kugomea rufaa kwa msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Katika posti za watu mbalimbali mitandaoni, waliandika kuwa Dr Cheki alisema Lulu ambaye ameanza maisha ya gerezani, alikataa ndugu zake wasikate rufaa kwa kile alichosema, anataka kumaliza kifungo chake mapema ili awe huru kisaikolojia. Lakini juzi, Dk Cheni ambaye alikuwa staa pekee aliyekuwa akihudhuria mahakamani wakati kesi hiyo ikifanyika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, alikanusha kuzungumza na Lulu, kwani hata siku ya hukumu hakuwepo kortini.
“Siyo kweli, mimi sijazungumza na Lulu tangu siku ile ya hukumu, kwanza sikuwepo mahakamani na hadi leo ninapoongea na wewe sijaenda kumtembelea gerezani, kwa hiyo hayo maneno siyo yangu,” alisema muigizaji huyo. Novemba 13, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimhukumu Lulu miaka miwili jela, baada ya kumkuta na hatia ya kuua bila kukusudia, kosa alilolifanya April 7, 2012 baada ya kuwa ndiye mtu wa mwisho kuwa chumbani na muigizaji mwenzake, marehemu Steven Kanumba aliyefariki siku hiyo
Tags
Burudani