CHANETA yaililia serikali

Chama cha mchezo wa pete nchini 'CHANETA' kimeiomba serikali kusaidia juhudi za kukuza mchezo huo kama ilivyo kwa michezo mingine nchini.

Akizungumza na www.eatv.tv, Mwenyekiti wa CHANETA, Devotha John Marwa amesema kuwa maombi yao kwa serikali kupitia kwa Wizara husika ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ni kuwa na vipaumbele vya kitaifa katika michezo, akiomba msaada wa ruzuku badala ya kuviachia vyama pekee.
"Mheshimiwa Waziri pale alipo kama ananisikia au wasaidizi wake, ni kwamba tunaomba serikali iweze kuwa na vipaumbele katika michezo, isiachie vyama pekee kwasababu vyama havina vyanzo vya mapato", amesema.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, "vyama vingi vinaendeshwa kwa kujitolea, ukikuta kama netiboli, yeye Waziri anajua kuwa chama tulivyokipokea hali ilikuwaje, hatukuwa hata na senti 5, hatukuwa hata na ofisi. Sasa ukiachia chama pekee kijiendeshe inakuwa ngumu", ameongeza.
Mafunzo
Aidha katika hatua nyingine, Bi Devotha amesema kuwa chama hicho kimeanzisha mafunzo ya kutoa elimu juu ya kuzifahamu sheria za mchezo huo, ambapo jumla ya sheria mpya 11 zimeongezwa tofauti na awali ambapo mchezo huo ulikuwa na sheria 21.
Mafunzo hayo yanatarajia kuanzia mikoani na baadaye kumalizia kwa  mafunzo ya kitaifa yatakayofanyikia mkoani Manyara, ambapo washindi wake wakitarajia kupewa vyeti.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post