Shkamoo Tshishimbi....Miguu iliyofunga Ndoa na Mpira


Fundi wa mpira. Mpaka rangi bora wa soka kwa muda huu. Kichaa wa soka kwenye kumiliki. Mkongo mwenye miguu iliyofunga ndoa na mpira. Akili kubwa kwenye dunia ya soka letu la afrika mashariki na kati.

Endelea kubishana kwa sababu hujamshuhudia au una kiburi . Ni mara chache sana mwanasoka kupendwa au kukubalika na pande mbili zote yaani Simba na Yanga.

Iliwatokea wachache sana. Kama Said Mwamba ‘Kizota’. Alipendwa na wana Yanga. Akakubalika kwa wana Simba. Kwamba huyu mtu ni fundi. Said alikuwa kama Juma Nature wa soka kwa wakati ule.



Ndivyo ilivyokuwa kwa kina Method Mogela. Hamis Gaga. Edibily Lunyamila na Juma Kaseja. Achana na Sunday Manara. Pamoja na upinzani mkali uliopo kwa timu hizi mbili. Marehemu Ben Luoga alikubalika kote kote. Simba walimpenda. Yanga wakamuhusudu.

Uchawi na ustaarabu kama siyo uhuni wa miguu yao. Ilikuwa chanzo cha kupendwa na kukubalika na kila pande za mashabiki wa timu hizi za Kariakoo. Walikuwa zaidi ya viingilio vilivyotolewa pale shamba la bibi.

‘Boban Mawela’ Haruna Moshi. Jibu utakalopewa na mashabiki wa Simba kuhusu uwezo wake. Litakuwa Kulwa. Na jibu utakalopewa na mashabiki wa Yanga kuhusu ufundi wake litakuwa Doto.



Yatafanana tu kwa kila kitu. Kuna uwezo wa soka wa mtu unamfanya hata shabiki wa timu pinzani ahusudu. Aheshimu na kumkubali mchezaji husika. Hakuna shabiki wa Manchester United aliyepinga uwezo wa Thierry Henry wa Arsenal katika ubora wake.

Kwa sasa hivi kuna mtu mmoja tu kwenye ligi kuu Tamzania Bara. Papy Kabamba Tshishimbi. Mkongomani huyu. Fundi wa mpira. Wakili halisi wa soka. Shahidi namba moja wa nini anatakiwa kufanya kiungo uwanjani.

Achana na blabla za wasemaji wa timu hizi. Huyu Tshishimbi siyo wa dunia hii. Ukimuangalia ni muunganiko wa Kizota Method na Gaga. Utaona robo ya ufundi wa Kizota. Robo ya ufundi wa Gaga na robo ya ufundi wa Method. Anajua sana huyu raia wa Kongo.




Ogopa sana mchezaji ambaye mashabiki wa timu pinzani wanatamani ashike mpira ili wafaidi ufundi wake. Anavutia kumtazama akichezea mpira kuliko ushindi wa timu yako.

Wakati Yanga wanaogopa Okwi asimiliki mpira kwa sababu atawaumiza muda wowote. Kuna kundi la mashabiki wa Simba litatamani Tshishimbi achukue mpira ili wafaidi kipaji halisi cha soka.

Haji Manara anakiri kuwa Tshishimbi ni mashine. Ndivyo ambavyo mashabiki wa simba sura zao zinadhihirisha kukubaliana na uwezo wa Tshishimbi. Jamaa anajua mpaka anakera.

Yanga wanaweza kuelemewa timu nzima. Lakini utamuona Tshishimbi tu uwanjani. Akipora mipira. Akigawa mpira. Akiomba pasi. Akiziba nafasi.

Hii siyo Bongo tu. Hata Ulaya mashabiki hukubali uwezo wa mchezaji wa timu pinzani. 2003 Old Trafford yote ilisimama kumpigia makofi mkongwe katika soka Ronaldo Nazario Luis De Lima.

Baada ya guu lake la kulia kutupia kambani goli tatu ndani ya dakika chache. Akimuacha Bathez na upara wake akilambalamba midomo kama zuzu. Ferguson akipata kigugumizi cha kutafuna jojo zake.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Ronaldinho pale Saintiago Bernabue. Baada ya kuwalaza na viatu mastaa wenye ustaa halisi wa Real Madrid. Wakati akitoka uwanjani majukwaa yote yalisikika makofi.

Heshima hii ya mashabiki kusimama majukwaani na kumpigia makofi mchezaji wa timu pinzani. Kwa hapa Bongo huo utamaduni umetuacha mbali sana. Haiwezi kutokea. Ila moyoni wataishia kukubaliana na hali halisi.

Kuna wakati unamtazama Tshishimbi. Unaona kama anawaonea wenzake au amelazimishwa kucheza nao. Anatuliza mpira tofauti na wenzake. Anapiga pasi tofauti na wenzake. Na hata namna anavyogeuka kutazama wapi apeleke mpira ni tofauti sana.

Ufundi huu ulikuwepo nyakati za kina Hussein Aman Masha. Marehemu James Tungaraza na kina Steven Mussa. Hawa ndiyo waliyokuwa wakifanya anayoyafanya Tshishimbi wa leo.

Lakini hawa wengine wanaopambwa kwenye vyombo vya habari. Ni wachezaji sawa. Lakini kwa Tshishimbi wa sasa ni kama mtende kuota katika ya Jangwa. Anaonekana peke yake uwanja mzima.

Naam hayo yalikuwa mawazo ya dk Levy

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post