Yanga yashusha vifaa 3 Jagwani




Kikosi cha timu ya Yanga.

KAMATI maalum ya kuweka mambo sawa Yanga inafanya mambo yake kwa usiri mkubwa lakini imebainika kwamba Kocha Mwinyi Zahera amewaambia anatua wiki ijayo na majembe matatu.

Zahera ambaye yuko mapumziko nchini Ufaransa, anafanya kazi kwa ukaribu zaidi na kamati hiyo, amewapa pia maelekezo kwamba wasimsainishe mchezaji yoyote yule mpya bila kumhusisha.

Habari kutoka ndani ya kamati hiyo iliyoko chini ya Abbas Tarimba zinasema kwamba Zahera amewadokeza kwamba wachezaji hao mmoja aliwahi kucheza soka la kulipwa nchini Israel na mwingine alikuwa kwenye kikosi cha mwisho cha DR Congo kilichocheza CHAN.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Jumamosi limedokezwa ni kwamba, majina halisi bado viongozi hawajakabidhiwa lakini wameambiwa kwamba mchezaji mmoja aliwahi kucheza Maccabi Haifa ya nchini Israel miaka ya nyuma.

“Watatua nchini siku yoyote kuanzia sasa lakini kuna jambo moja ambalo kocha amewaambia viongozi kuwa kabla ya kuwapatia mikataba itabidi kwanza viongozi wengine wa benchi la ufundi la timu hiyo wawaone kwanza uwanjani,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza kuwa.

“Kuna wachezaji wengi wawili kutoka nchini Zambia, pia watakuja kwa ajili ya majaribio nao wanatua kabla ya Juni 25,” alisema huku akidai kwamba kwa hali ilivyo mpaka sasa wameshapata uelekeo wa kikosi kijacho kitakavyokuwa.
Habari zinasema kwamba kamati ya Yanga imepanga kusajili kikosi cha wastani chenye wachezaji wazoefu ambao wanaweza kufanya vizuri ligi ya ndani na Kombe la FA.

Kigogo mmoja ndani ya Yanga amesisitiza kwamba wameamua kufanya usajili huo kwa kutulia kutokana na hali halisi ya kiuchumi pamoja na aina ya mashindano wanayoshiriki mwakani ambayo ni ya ndani tu.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa jana hakutoa ushirikiano kufafanua usajili huo na jinsi mambo yanavyokwenda ndani ya Yanga kwa sasa lakini Tarimba alizungumza kitu kizuri kwa mashabiki wa timu hiyo.

Tarimba ambaye ni kiongozi wa juu wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa, ni miongoni mwa vigogo wa kamati hiyo iliyoundwa na Yanga yenye wajumbe 12 kuhakikisha mambo yanakwenda sawa wakati wakiendelea kumshawishi Yusuf Manji arejee Jangwani.

Alisema wanahitaji kurejesha heshima ya Yanga kwa kuhakikisha wanasajili kikosi bora na usajili huo utafanyika kimyakimya kwa hofu ya kuingiliwa na wapinzani wao.

“Wanayanga wasiwe na wasiwasi tutafanya usajili makini ambao utaisaidia timu kufanya vizuri katika mashindano yote, tutamkimbiza mwizi kimyakimya hatutaweka wazi mipango yetu,” alisema Tarimba.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post