Yanga imeshaanza tizi tangu juzi Jumanne, lakini pia benchi lake la ufundi linawajaribu wachezaji 14 waliofika kuomba kazi Jangwani.
Wachezaji hao ni pamoja na kiungo mmoja rasta kiraka aliyetua sambamba na mshambuliaji mmoja mtukutu.
Katika mazoezi hayo yanayofanyika katika Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam, kiungo mpya aliyetua na kuanza mambo ni Jafar Mohammed aliyeitumikia Majimaji msimu uliopita.
Yanga ilikuwa ikimwinda Jafar muda mrefu tangu akiwa Toto Africa ya Mwanza kabla ya kushuka daraja na sasa wamemshusha mazoezini kuangaliwa na kocha Mwinyi Zahera.
Kushushwa kwa Jafar kunatokana na Zahera kuwaambia mabosi wa Yanga anataka atafutiwe beki wa kushoto kiraka anayejua kucheza nafasi nyingi ambapo akili ya kwanza ya wakuu hao wa Yanga ikatua kwa rasta huyo.
Jafar anamudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na hata beki wa kushoto kutokana na kujua kutumia vyema mguu wake wa kushoto na tayari sasa anapimwa na kocha Zahera kujua hatma yake.
Mbali ya Jafar jina jingine kubwa ni mshambuliaji, Cosmas Lewis ‘Baloteli’ ambaye jana alionekana katika mazoezi ya Yanga akijaribu bahati yake.
Mshabuliaji huyo mkongwe mtukutu jana alikuwa sehemu ya mazoezi ya Yanga, huku nje akiwa meneja wake Herry Mzozo aliyekuwa akishuhudia mazoezi hayo.
MBENIN NUSURA AZIMIE
Katika mazoezi hayo Zahera aliwakimbiza wachezaji wake kwa zaidi ya dakika 40 na mshambuliaji Marcelin Koupko alikutana na dozi hiyo kubwa na jamaa ikamlazimu kuchagua kasi yake ili asiishie njiani.
Koupko alianza vizuri mazoezi hayo, lakini kadiri ya muda ulivyosogea alishindwa kutunza ubora wake na kujikuta akibaki wa mwisho huku wenzake wachache wakipeta.
Kiungo Papy Kabamba Tshishimbi, mshambuliaji Heritier Makambo na kiungo Yahya Akilimali ndio waliofanikiwa kumudu aina hiyo ya mazoezi wakimaliza wakiwa vinara.
Katika tizi la jana wachezaji zaidi ya 14 wakiwamo wageni walifurika kutesti zali mbele ya Mkongomani Zahera aliyekuwa akiwaangalia kabla ya kuamua hatma yao kwa ajili ya usajili mpya wa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbali ya ushiriki wao kwenye mashindano hayo pia inataka kuwa na kikosi imara ili msimu ujao iweze kulirejesha taji la Ligi Kuu Bara lililoenda Msimbazi.
Yanga inatarajia kuifuata Gor Mahia ya Kenya mwezi ujao kabla ya kurudiana nayo siku wiki moja baadaye jijini Dar es Salaam katika mechi zao za makundi ya michuano hiyo.
Timu hizo zipo pamoja na vinara USM Alger ya Algeria na Rayon Sports ya Rwanda.