Wakati viongozi wa Yanga wakiwa wanafanya jitihada za kuinasa saini ya kiungo wa Ndanda FC ya Mtwara, Mrisho Ngassa, kiungo huyo ameibuka na kuweka wazi kwamba kwa sasa anachosubiri ni kuona anaingia mkataba na timu hiyo kama wataafikiana kwenye mazungumzo yao ambayo wanaendelea kwa sasa.
Ngassa amekuwa chaguo la viongozi wa Yanga wakitaka wamjumuishe tena kwenye kikosi chao baada ya kiungo huyo kuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Ndanda FC kusalia kwenye ligi kwa msimu ujao wa 2018/19.
Kiungo huyo ambaye pia kwa nyakati tofauti amezichezea Simba na Azam FC, ameliambia Championi Jumatatu, kwamba kwa sasa anaendelea kuzungumza na viongozi wa Yanga kwa ajili ya yeye kutua ndani ya klabu hiyo na kama mambo yakienda sawa, muda wowote atakuwa tayari kumwaga wino.
“Bado sijasaini mkataba wowote ule, ninaendelea tu na mazungumzo na Yanga na kama tukiafikiana, basi nitajiunga nao kwa sababu mimi ni mchezaji, kokote pale ninaenda kufanya kazi bila ya kuchagua ni wapi.
“Lakini pia siyo Yanga tu ambao nafanya nao mazungumzo, kuna timu nyingine nazo zipo japo siwezi kuziweka hadharani ni zipi ila naongea nazo pia, kwa yoyote ambayo itaafikiana na mimi basi ndiyo hiyo ambayo nitakuwa nayo kwa msimu ujao,” alisema Ngassa.
Ngassa ni moja ya nyota ambao wanatakiwa na Yanga kwa ajili ya kujiimarisha kwa msimu ujao, pia klabu hiyo inawafuatilia wachezaji Juma Nyosso wa Kagera Sugar, Pascal Wawa kutoka Ivory Coast na kipa Ley Matampi anayetokea DR Congo huku ikimalizana na straika Marcelin Koukpo.
CHANZO: CHAMPIONI