Mambo yanasinga mbele na Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Congo, Zahera Mwinyi amekwamisha usajili mpya wa kiungo wa pembeni wa timu hiyo Geofrey Mwashiuya kutaka kujiunga na Nkana FC ya Zambia.
Tayari Mwashiuya alipata dili Zambia, wakati akiana kufanya mchakato, Zahera akazungumza na viongozi wanaohusika na usajili na kusisitiza “ana kazi na Mwashiuya”.
Mkataba wa Mwashiuya kuitumikia Yanga ulifikia kikomo mwishoni mwa msimu uliomalizika na kumfanya kuwa huru jambo ambalo yeye alianza rasmi kusaka timu mpya ya kuitumikia ambapo tayari timu ya Nkana ya Zambia ambayo ipo kwenye nafasi ya nane katika msimamo wa ligi kuu ya nchi hiyo imemtangazia dau la shilingi Milioni 28 ili imsajili.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa pamoja na Mwashiuya kuhitaji kwenda nchini Zambia, anashindwa kuchukua uamuzi huo mapema kutokana na maagizo ya Kocha Mkuu wa Yanga Zahera Mwinyi kuwataka viongozi wa timu hiyo wasimruhusu kuondoka kwani bado anahitaji huduma yake msimu ujao.
“Kweli Mwashiuya kapata timu Zambia tena ipo ligi kuu ya nchi hiyo na kwa macho yangu niliwaona walipokuja kumfuata Mbeya ambapo walikubaliana hadi kiasi cha cha kumsajilia ambapo walianza kwa kumtaka achukue milioni 28 lakini yeye akawambia wamsubirie atawajibu kutokana na kocha wa Yanga kama atamruhusu kuondoka kwani viongozi wake walimwambia asiondoke maana kocha amependekeza jina lake,” kilisema Chanzo hicho.
Baada ya kusikia hivyo lilimtafuta Mwashiuya mwenyewe ili azungumzie madai hayo ambapo alisema: “Ni kweli nimeshafanya mazungumzo na timu ya Nkana ya Zambia, maana walikuja hadi hapa Mbeya wakanipigia tukakutana wakanitajia dau lao ambalo kweli siyo baya sana kwangu kipindi hiki ambacho nipo huru.
“Ninawasikilizia kwanza viongozi wangu wa Yanga maana waliniambia nisikurupuke kwenda mahali kwa sasa kufuatia maagizo ya kocha wetu kwani alisema bado ananihitaji hivyo kama ofa ya Yanga itakuwa nzuri kuliko hii nitaendelea Yanga ila ikionekana ya kawaida nitaenda kujaribu changamoto mpya huko Zambia,” alisema Mwashiuya.