SIMBA MPYA YA MO DEWJI YAFANYA KUFURU USAJILI HUU


SIMBA walianza kumsainisha Marcel Kaheza wa Majimaji, akafuatia Adam Salamba wa Lipuli. Mashabiki wakaguna…aaah jamaniieee watacheza wapi wote hao mastraika?

Huku na huku mara wakamshusha tena Mohammed Rashid wa Prisons, Yanga wakaibuka wakaaanza kulalamika kwamba Simba wanatibua tu michongo yao makusudi kwa vile wana mkwanja.

Wadau walikuwa wakigunia usajili wa mastraika hao watatu kwa vile wote wana sifa zinazokaribiana na waliongoza kwenye timu zao msimu uliopita. Salamba alikuwa na mabao sita pale Lipuli, Rashid alikuwa na 10 huko Prisons na Kaheza 14 pale Majimaji.

Kumbe bwana hicho kilichofanyika siyo bahati mbaya ni mipango matata sana ya mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ kuhusiana na usajili mpya wa kikosi hicho msimu ujao.

MO amewaambia viongozi wa Simba kwamba usajili wa msimu ujao anataka uwe wa tofauti sana na ndiyo maana utafanyika na watu wachache sana akiwemo yeye na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘try again’ chini ya muongozo wa ripoti ya makocha.

Kiongozi huyo anayefahamika Afrika nzima kwa utajiri na mbinu za ujasiriamali amewaambia vigogo wa Simba kwamba anataka kila nafasi uwanjani iwe na wachezaji wawili imara sana yaani aliyeko kwenye benchi awe mkali kuliko aliyeanza ili iwe bandika bandua.

Championi Jumatano, limebaini kwamba huku akiendelea kusuka kikosi hicho tayari mazungumzo baina yake na makocha kadhaa kutoka Ulaya Kaskazini na Ubelgiji anaotaka waje kuinoa Simba yamefikia pazuri lakini ni siri kubwa hata viongozi wengine hawajui ni nini kinaendelea.

“Kila nafasi anataka iwe na wachezaji imara sana yaani kwenye benchi kuwe na straika mkali kuliko Okwi na Bocco. Na anataka hilo lifanyike kwenye nafasi zote, kuwepo na vikosi viwili imara sana ambavyo havitazuilika kwenye ligi za ndani na michuano ya kimataifa.

“Lakini hao wachezaji imekuwa ni siri sana anafanya yeye na Salim, hakuna yale mambo ya kamati kama zamani,”alidokeza kiongozi mmoja wa Simba ambaye aliongeza kwamba hata Obrey Chirwa wa Yanga alikuwa kwenye mipango yao lakini wamesikia amepata dili Misri katika klabu kongwe ya Ismailia,” kilisema chanzo hicho.

Habari za ndani zinasema kwamba MO ambaye ni Simba wa kulia machozi hatumii tena kamati maalum ya usajili kama ilivyokuwa siku za nyuma ndio maana mambo mengi yanakwenda kwa siri sana na habari zinasema amekuwa akisisitiza hivyo pia ili kuepuka ‘cha juu’.

Habari zinasema kwamba viongozi wengi wa Simba ambayo imeshampiga chini straika kipenzi cha msemaji wa Simba, Haji Manara, aitwae King Laudit Mavugo wameafiki anachofanya MO kwa sasa kwenye usajili kwani kitajenga timu imara ambayo itakuwa na ushindani mkubwa na itawasaidia kuonyesha mabadiliko ambayo yameanza kuonekana kwenye uendeshaji.

Habari zinasema kwamba MO amepania kusajili mchezaji wa gharama yoyote ndani ya Afrika na hata kwenye mkutano mkuu wa wanachama alithibitisha hilo na kupigiwa makofi yenye kilo nyingi.

Simba ambayo itashiriki michuano ya Kagame inayoanza Juni 29, Jijini Dar es Salaam, inajiandaa pia na Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Desemba mwaka huu badala ya Februari kama ilivyozoeleka.

Baadhi ya timu ngumu za Afrika ambazo mpaka sasa zimefuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni pamoja na Esperance na Club African za Tunisia, Al Ahly na Ismailia zote za Misri.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post