CHIRWA KUWEKA REKODI SIMBA


USAJILI mpya wa Ligi Kuu Bara haujafunguliwa rasmi lakini Simba tayari imeshaweka rekodi. Simba chini ya udhamini wa bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ tayari imesajili mastraika watatu kwa mpigo na wote wakiwa ndiyo wafungaji bora katika timu zao msimu uliopita.

Lakini kama wakifanikiwa kukamilisha usajili wa straika wa Yanga, Obrey Chirwa ambaye wanataka azibe nafasi ya Laudit Mavugo ambaye ameshatemwa, itaweka rekodi kubwa zaidi.

Wachezaji watatu ambao Simba imeshamalizana nao wameibua gumzo la jinsi watakavyocheza ndani ya kikosi hicho ni Adam Salamba aliyekuwa na mabao sita Lipuli, Mohamed Rashid aliyekuwa na 10 Prisons pamoja na Marcel Boniventure aliyetupia 14 ndani ya Majimaji.

Katika wachezaji hao watatu ambao kila kitu chao kimeshakamilika hata kabla ya dirisha kufunguliwa Juni 15, Boniventure na Rashid wako kwenye nafasi tano za juu za msimamo wa wafungaji wa msimu uliopita.

Lakini kama Simba ikifanikiwa kumnasa Chirwa ambaye yuko kwenye mazungumzo mazito na timu moja ya Misri, itakuwa imeweka rekodi mpya ya kusajili mastraika wote waliokuwa kwenye tano bora msimu uliopita.

Kwenye msimamo wa ufungaji bora msimu uliopita, Emmanuel Okwi ambaye ni mali ya Simba ndiye kinara kwa mabao yake 20 akifuatiwa na John Bocco ambaye pia yuko Msimbazi akiwa na mabao 14. Wengine watatu wanaofuatia ndiyo hao ambao Simba imewaweka sawa.

Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna alisema; “Mapendekezo ya mwalimu ndiyo tunayotumia kusajili kwa kuwa timu haiwezi kufanya usajili bila kupokea ripoti hivyo kikubwa tumeanza na hawa wachezaji kwa kuwa usajili bado unaendelea na mipango mizuri inaendelea na kwa kufanya hivyo kutasaidia kufanya vizuri kimataifa.”

“Tuna michuano mingi ambayo tutashiriki kwa sasa kuna Kagame, Klabu Bingwa Afrika na Ligi hivyo mahitaji yetu ni kufanya vizuri kwenye mashindano hayo pia imani yetu ni kuweza kuleta ushindani kimataifa,” alisisitiza Kajuna kwa kusema kwamba hawajasajili mastraika hao kwa bahati mbaya.

CHANZO: SPORTEXRA

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post