YAMETIMIA: HATIMAE NGOMA AELEKEA AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU



Na George Mganga

Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Donald Ngoma, ameondoka usiku wa kuamkia leo majira ya saa 9 kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya.

Ngoma aliyesajiliwa na Azam kutoka Yanga, amesafirishwa kuelekea jiji la Cape Town ili kupata vipimo vya afya ili kuona tatizo lipi linalomsumbua.

Kwa mujibu wa Ofisa wa Habari wa Azam FC, Jaffar Maganga, amesema kuwa watakuwa tayari kumgharamikia Ngoma endapo itabainika ana tatizo katika afya yake na kama atakuwa yuko sawa atarejea nyumbani.

"Kama Ngoma atabainika ana tatizo lolote katika mwili wake, klabu ya Azam itawajibika kutumia gharama zozote zile kwa ajili ya matibabu yake. Na kama ikitokea yuko sawa, atarejea nchini" alisema.

Ikumbukwe Ngoma wakati akiwa Yanga hakucheza takribani msimu mzima wa 2017/18 kutokana na kusumbuliwa na majeruhi, hivyo ilisababisha asionekane Uwanjani kwa muda mrefu.

Ngoma ambaye ni raia wa Zimbambwe, alisajiliwa na Azam kwa kusaini mkataba wa miaka miwili ambapo alijiunga na Yanga kutokea FC Platnumz ya nchini kwao mwaka 2015.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post