SIKU ZA YONDANI YANGA ZINAHESABIKA, MCHONGO KAMILI UPO HIVI


Wakati mashabiki wa Yanga wakipigwa na butwaa kusikia, straika wao Donald Ngoma akitua Azam siku chache baada ya mabosi wao kumtupia virago, siku za beki kisiki wa timu hiyo na Taifa Stars, Kelvin Yondani zinaanza kuhesabika klabuni hapo.

Yondani anayetumikia adhabu ya kosa la kumtemea mate beki wa Simba, Asante Kwasi yupo njiani kuitema Yanga kama mabosi wake, hawatafanya maarifa mapema ili kumsainisha mkataba mpya kabla mambo hayajaharibika.

Inaelezwa kuwa, beki huyo aliyetua Yanga akitokea Simba mwaka 2012 yupo katika mazungumzo ya siri na klabu za Simba na Azam kutokana na mkataba wake wa sasa kumruhusu kuzungumza na klabu yoyote.

Beki huyo aliwahi kunukuliwa na Mwanaspoti kuwa klabu za Simba na Azam zimemwekea ofa nono mezani, lakini alikuwa akiwasikilizia mabosi wake wa sasa kama watamalizana naye mapema ili asaini kuendelea kuichezea Yanga.

Hata hivyo, mambo ni kama bado hayajakaa sawa na Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alikiri mabosi wa Jangwani wanapambana kuhakikisha wanambakisha beki huyo wa kati.

Hafidh alisema Yondani kamaliza mkataba na Yanga na ametoa nafasi kwa uongozi kukaa naye ili aweze kuendelea kuitumikia timu hiyo kama wapo tayari kumtimizia mahitaji yake anayoyataka.

“Kinachosubiriwa sasa ni nafasi aliyotoa Yondani uongozi kuifanyia kazi la sivyo beki huyo huenda ataondoka kwenda klatika timu nyingine ambazo zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake tayari kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.

Hafidh alisema Yondani alishawaambia walipokutana mapema mezani kwamba Simba na Azam wameonyesha nia ya kutaka huduma yake lakini anawasilikizia mabosi wake wa sasa la sivyo atawapa mkono wa kwaheri.

Katika hatua nyingine Meneja huyo alifichua kuwa, Kocha Mkuu wao, Mwinyi Zahera, anatarajia kurudi nchini kuanzia kesho Jumatatu mara baada ya pambano la DR Congo na Nigeria ili aanze majukumu yake kwa michuano ya SportPesa Super.

Credit: MwanaSpoti

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post