KIPA WA LIVERPOOL ATISHIWA MAISHA


Polisi wa eneo la Merseyside, Uingereza wamesema wanafahamu kuhusu vitisho vya maisha ambavyo vimetolewa dhidi ya mlinda lango wa Liverpool Loris Karius baada ya kuchezwa kwa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumamosi.

Maafisa wamesema vitisho vyovyote vinavyotolewa kupitia mitandao ya kijamii vinafaa kuchunguzwa.

Karius, 24, na familia yake wamekuwa wakipokea vitisho baada ya makosa mawili kutoka kwake kuwasaidia Real Madrid kupata ushindi wa 3-1.

"Tunachukulia ujumbe huu wa vitisho kwenye mitandao ya kijamii kwa uzito sana. Visa hivi vitachunguzwa," polisi wamesema.

"Maafisa wa polisi wanafahamu kuhusu ujumbe kadha na vitisho vilivyotolewa kupitia mitandao ya kijamii.

"Polisi wa Merseyside wangependa kuwakumbusha wanaotumia mitandao ya kijamii kwamba makosa yooyte yakiwemo kutoa mawasiliano yenye hila na kutumia vitisho, haya yote yatachunguzwa."

Mjerumani huyo alimpa mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema bao rahisi la kwanza mjini Kiev.

Baadaye, alimruhusu Gareth Bale kufunga bao la tatu la Real kutoka mbali alipojaribu kuzuia kombora lake lakini likapita mikono yake na kutumbukia wavuni.

Hilo liliwawezesha Real kushinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia.

Baada ya kipenda cha mwisho kupulizwa, mlinda lango huyo alionekana kusikitika na kutokwa na machozi.

Baadaye, aliwaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo ya Anfield.


Loris Karius alifanya makosa mawili kwenye fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya

Liverpool wana nyenzo za kumsaidia Karius - Mignolet

Mlinda lango mwenzake Liverpool Simon Mignolet amemtetea Karius na kusema atajikwamua kutoka kwa masaibu hayo ya fainali hiyo ya Uefa.

"Iwapo anataka kuzungumza, bila shaka nitakuwepo," alisema Mbelgiji huyo aliyekuwa kwenye benchi wakati wa mechi hiyo.

"Kila kipa anamuelewa.

"Nimewahi kujipata katika hali kama hii mwenyewe awali na hayo ni mambo ambayo huwa unakumbana nayo.

"Kitu pekee nilichomwambia ni kwamba kuna sababu iliyotufanya kufika fainali, na kuna sababu yetu kucheza kwenye fainali, hivyo fikiria hilo.

"Lakini bila shaka, ni jambo ngumu sana kumwambia chochote na kumwacha atulie na kuelewa.

"Liverpool husimamia umoja, Liverpool husimamia 'sote kwa pamoja'. Nafikiri hilo halitakuwa tu kwamba ndilo jambo bora kwa Liverpool, bali imekuwa ndiyo historia yao na itasalia hivyo sku za baadaye."

Mkufunzi wa makipa wa Liverpool John Achterberg alijaribu kumliwaza Karius baada ya mechi hiyo.

"Bila shaka kilichotokea hakikuwa kitu kizuri. Ilikuwa mkosi kwake kwamba ilitokea wakati wa mechi hii," alisema Mholanzi huyo.

"Nilijaribu kuinua kichwa chake na kumuonesha kwamba tunafaa kusonga mbele. Ni vigumu lakini hayo ndiyo maisha katika soka."

Beki Dejan Lovren alisema haitakuwa na faida yoyote kumlaumu karius.

Ni rahisi sana kumlaumu mtu, lakini tupo kwenye meli hii pamoja na kila mtu alitoa maneno mazuri kwake kadiri tulivyoweza. Atajikwamua," Lovren alisema.

"Msiandike hadithi kubwa na ndefu kuhusu hilo. Ni kweli kwamba ni kubwa kwa sababu ilikuwa fainali, lakini hakuna asiyefanya makosa."


Loris Karius alihamia Liverpool kutoka Mainz ya Ujerumani kwa £4.7m Mei 2016

Karius mwenyewe amesema "anaomba radhi bila kipimo" baada ya makosa yake.

"Najua kwamba nilikosea sana kwa makosa yangu hayo mawili na niliwavunja moyo nyote," aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

"Kusema kweli, sijapata usingizi hadi sasa," aliandika baada ya mechi.

"Yaliyotokea bado yanapitia kichwani mwangu tena na tena.

"Nawaomba radhi bila kipimo wachezaji wenzangu, nanyi mashabiki, na kwa wafanyakazi wote wa klabu.

"Ningelipenda sana kusongeza nyuma mshale wa saa lakini hilo haliwezekani.

"Inauma zaidi kwani sote tulihisi kwamba tungewalaza Real Madrid na tulikuwa tunacheza vyema kwa muda mrefu.

"nawashukuru sana mashabiki waliofika Kiev na kuniunga mkono, hata baada ya mechi.

"Sitalisahau hilo na kwa mara nyingine tena lilinionyesha jinsi tulivyo kama familia moja kubwa. Asanteni, na tutaerejea tukiwa na nguvu zaidi."

Ninamuonea huruma sana - Klopp

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp, ambaye bado hajashinda kikombe tangu ajiunge na Liverpool 2015 amesema anamuonea huruma sana karius.

"Kosa hilo la pili lilitokea kwa sababu ya lile la kwanza. Ni vigumu sana kuzifuta fikira hizo mbaya kutoka akilini mwako," alisema.

"Loris anajua hilo, kila mtu anajua. Ni aibu sana kutokea katika mechi kama hii, katika msimu kama huu.

"Namuonea huruma sana. Yeye ni mchezaji mzuri."

'Tukishinda tunashinda kama timu, tukishindwa, kama timu pia'

Nahodha wa Liverpool Jordan Henderson alikataa kulaumu makosa ya Karius kwa kushindwa kwa Liverpool kwenye fainali hiyo.

Liverpool walikuwa pia wameshindwa fainali Kombe la Ligi Uingereza na Europa League 2016.

Ushindi wao wa mwisho fainali ulitokea jijini Cardiff kwa mikwaju ya penalti fainali ya Kombe la Ligi Uingereza 2012.

"Si makosa yaLoris Karius, tulifika fainali kama timu na tulishindwa kama timu. Ni kuhusu kila mtu. Uchezaji wetu haukutosha siku hiyo."

'Itamchukua miezi mitatu hivi kusahau'

Mwnaasaikolojia wa michezo Dkt Steve Peters, ambaye amewahi kufanya kazi na timu ya taifa ya England anasema Karius atahitaji muda kuyasahau makosa yake.

"Hii ni michezo na siku moja mambo wakati mwingine huenda mrama. Jambo muhimu zaidi ni kukubali kwamba hajapoteza kipaji chochote au uwezo wowote. Ni makosa kadha tu, kwa hivyo vyema zaidi huwa kukubali ukweli. Huenda asiwahi kurudia makosa hayo tena.

"Kwa kawaida, itamchukua miezi kama mitatu hivi kwake kukubali kwamba hayo yalipita. Hatujui ni kwa sababu gani huchukua muda kama huo - akili huchukua muda kutafakari na kulikubali jambo. Kwa usaidizi wa wataalamu, hili linaweza kufanikiwa hivi kwamba mwishowe unatokea ukiwa hata na nguvu zaidi badala ya kukudhoofisha."

Kipa wa zamani wa Ray Clemence, aliyeshinda Kombe la Ulaya akiwa na Liverpool kati ya 1977 na 1981, anasema kipindi cha mapumziko ya majira ya joto kitakuwa kirefu sana kwa Karius ambaye hakutajwa kikosi cha Kombe la Dunia cha Ujerumani.

"Alifanya makosa mawili makubwa wakati muhimu kwenye mechi na itamulazimu kuishi na hilo maisha yake yote," kipa huyo wa zamani wa England Clemence aliambia BBC Radio 5.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post