MO DEWJI KUAMUA HATMA YA KIONGOZI HUYU WA SIMBA



NI dhahiri msimu ujao Simba hawatakuwa na kocha wao, Pierre Lechantre na sasa jukumu la kushusha mtu sahihi atakayebeba mikoba ya Mfaransa huyo amekabidhiwa bilionea wao, Mohamed Dewji ‘Mo’.
Taarifa za kuaminika kutoka Simba zinadai kuwa, pande hizo mbili zimeshindwa kuafikiana juu ya mkataba mpya na kocha huyo atamalizia tu mchezo wa kesho wa funga dimba dhidi ya Majimaji na baada ya hapo atafungasha kila kilicho chake.
Simba wamepata taarifa kuwa, Mfaransa huyo ameshapeleka barua za kutaka kibarua katika timu ya Taifa ya Cameroon na wenyewe wameona isiwe shida na badala yake wameamua kumfungia vioo, ikizingatiwa kuwa, anataka kulipwa mshahara mkubwa.
Taarifa zaidi zinadai kuwa, baadhi ya viongozi hawaridhishwi na aina ya soka ambalo analifundisha, likionekana la kujilinda zaidi, licha ya kuwa na wachezaji wenye kasi ambao wana uwezo wa kucheza mpira wa kasi na kupata mabao ya kutosha.
Baadhi ya vigogo hao pamoja na mashabiki wamekuwa wakimshutumu Mfaransa huyo kuwa katika michezo ya hivi karibuni timu imekuwa ikishindwa kupata ushindi mnono na hata kufikia hatua ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar, kisa kikiwa kuhusudu soka la kujilinda zaidi.
Wenye timu yao wanadai kuwa, awali kikosi kilivyokuwa chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma, kilikuwa kikicheza soka safi la kisasa lenye pasi za uhakika na pia wachezaji walikuwa wakifunga idadi kubwa ya mabao, lakini Mfaransa huyo alipokabidhiwa majukumu mambo yakabadilika.
Kutokana na hali hiyo, taarifa zinadai kuwa, baada ya mchezo wa kesho kumalizika, kocha huyo ataondoka na timu itakuwa chini ya Masoud, katika michuano ya SportPesa inayotarajiwa kufanyika nchini Kenya na baadaye wataangalia uwezekano wa kumleta kocha mpya.
Taarifa hizo zinadai kuwa Mo Dewji amekabidhiwa jukumu la kuhakikisha anamleta kocha mwenye viwango vitakavyoifanya timu ichukue kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kama walivyoshauriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, wakati akiwakabidhi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post