Baada ya klabu ya Simba kukamilisha usajili wa Adam Salamba aliyemaliza mkataba na Lipuli, msemaji wa mabingwa wa VPL Haji Manara amesema usajili utakaofuata itakuwa ni pigo takatiu.
Manara amesema Simba itakwenda Nairobi kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup na mchezaji ambaye usajili wake utakuwa tishio.
“Yatakayokuja yatakuwa yanafurahisha, itakuwa ni pigo takatifu. Sisi tumefundishwa kisasi ni haki, vilevile tulivyofanyiwa na sisi tutafanya, hatuwezi kuwaacha lazima tulipe”-Manara ameiambia Sports HQ.
“Timu inatua leo tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, tutakwenda na mtu wa kustua itakuwa tishio.”
“Wakati ule walitufanyia sisi, kila mchezaji mzuri walikuwa wanamchukua sasa ni muda wetu tutalipa kila pigo tulilopigwa linalipwa hapahapa duniani tena mwaka huu.”
Manara hajaweka wazi ni mchezaji gani anaetarajiwa kutua Msimbazi hivi karibuni na alipoulizwa kama mchezaji huyo anatoka kwa watani zao Yanga jambo hilo litafahamika baadaye lakini wao watalipa kisasi.
“Kama kuibomoa Yanga hiyo tutajua baadaye lakini kisasi ni haki waliofanya ndio wanajua, tutalipa kwa nguvu ileile tena inawezekana tukazidisha ili maumivu yawapate mara tano yake. Hiyo ndo habari ya mjini.”
“Sisi tunasajili kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi lakini mapendekezo hayo yanakwenda sambamba na siasa za mpira lazima tukubali hilo jambo. Siasa za mpira zipo dunia nzima ndioaana kuna wakati anachukuliwa Neymar kutoka Barca kwenda PSG zile ni siasa tu za soka.”
“Tunakwenda kucheza klabu bingwa Afrika, tukiona mchezaji mzuri kwenye timu yoyote tutamchukua ndani ya Tanzania na nje ya mipaka yetu.”
Inaelezwa kuwa, Simba huenda ikamsajili mshambuliaji wa Yanga Obrey Chirwa katika kipindi hiki.