Kuelekea mchezo wa VPL kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Yanga, Kocha mkuu wa Prisons Abdallah Mohamed ‘Bares’ ameivua ubingwa Yanga na kuipa Simba nafasi ya kushinda taji la ligi kuu msimu huu.
Bares amesema Simba inahitaji pointi moja kuwa bingwa wa ligi huku ikiwa na mechi tatu jambo ambalo linaiondoa Yanga katika mbio za ubingwa wa VPL 2017/18.
“Tunaona tayari Yanga ameshaondoka kwenye mbio za ubingwa kwa sababu Simba anahitaji pointi moja kuwa mabingwa, mchezo dhidi ya Yanga ni muhimu sana kwetu kupata pointi tatu.”
“Nadhani Yanga wanakuja wakiwa wanajiandaa zaidi kwa mechi yao ya kimataifa, huu utakuwa mchezo wa kuandaa mazoezi ambayo yatawasaidia na mapungufu ambayo wameona kwenye mchezo waliofungwa 4-0 USM Alger. Nadhani kikubwa mwalimu atatazama hicho zaidi.”
“Kikosi changu kipo vizuri isipokuwa tutamkosa mchezaji mmoja Salum Kimenya ambaye anakabiliwa na kadi tatu za njano kwa hiyo hatutaweza kumtumia lakini tuna vijana wengi ambao wako vizuri na tunaamini watafanya vizuri.”
“Kila timu imejipanga kwa namna yake, sisi tumejipanga kukamata nafasi za juu nadhani Yanga kama kawaida yake haitaki kushuka chini zaidi inataka kubaki palepale nadhani mchezo utakuwa ni mkubwa lakini tuangalie dakika 90 zitaamua nini.”
“Tunacheza na Yanga ambayo jina lake ni kubwa lakini timu ya kawaida kabisa, sisi kama unavyoona mwenendo wetu sio mbaya kwa hiyo tunataka kuendeleza hiyo rekodi yetu.”
Tags
LIGI KUU VPL