Timu hiyo ya Jijini Mwanza ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi lao C kwa kuvuna pointi 28 pamoja na Biashara United walioongoza kwa alama 30.
MWANZA. MAMBO ni moto unaambiwa, baada ya kufanikiwa kupanda Ligi Kuu kwa timu ya Alliance FC, imemnasa Kocha Papii Kailanga atakayekinoa kikosi hicho msimu ujao.
Timu hiyo ya Jijini Mwanza ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi lao C kwa kuvuna pointi 28 pamoja na Biashara United walioongoza kwa alama 30.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Klabu hiyo,Yusuph Budodi alithibitisha kutua kwa Papista ambaye alikuwa Kocha Msaidizi wa kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda na kwamba lengo la kumleta kikosini humo ni kuhakikisha timu inafanya vizuri msimu ujao.
Alisema kuwa Kailanga amepewa kandarasi ya mwaka mmoja na kuongeza kuwa uongozi utakaa na kuamua kati ya Mnyarwanda huyo na Mbwana Makata nani atakuwa Kocha Mkuu.
“Tumeongeza nguvu kwenye benchi la ufundi kwa kumleta Kocha mpya aitwaye Papii Papista Kailanga ambaye alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Rwanda, kujua nani atakuwa kocha mkuu hilo uongozi utaamua baadaye,” alisema Budodi.
Budodi aliongeza kuwa tayari timu imeanza kambi kwa wachezaji walioipandisha daraja na kwamba wengine wataanza kuwasili baada ya siku mbili wakiwamo wa kigeni kuja kufanya majaribio.
“Mpaka sasa wachezaji walioipandisha timu daraja wapo kambini na wengine wanatarajia kufika ndani ya siku mbili wakiwamo wa kigeni ambao wanakuja kwa majaribio,” alisema Budodi.