DEJAN LOVREN MKIMBIZI WA VITA ANAYEPANGA KUMZIMA CRISTIANO RONALDO FAINALI UEFA


“Mungu hakupi unachokitaka bali anakupa unachokitafuta” huu ni moja ya mstari uliopo katika nyimbo ya nguli wa Rap nchini Tanzania Fareed Kubanda aka Fid Q, napata mawazo ya mstari huu baada ya kusikia story ya mlinzi wa kati wa Liverpool Dejan Lovren alivyokimbia vita hadi sasa anavyokwenda kucheza fainali ya Champions League.
Mwaka 1989 ndio mwaka mlinzi huyu alipozaliwa lakini machafuko nchini kwao Yugoslavia yalimfanya mama yake mzazi aitwaye Silva na baba yake Sasa kumbeba mtoto wao na kukimbia naye kuelekea nchini Ujerumani kutafuta hifadhi.
Ilikuwa mwaka 1992 ambapo wazazi wake waliamua kuondoka Yugoslavia katika eneo liitwalo Zenica na kukimbilia Ujerumani ambako hawakuwa wakimfahamu mtu hata mmoja, mwaka mmoja tu baada ya Lovren kukimbia Zenica kulitokea shambulizi la kivita ambalo lilua watu wengi na Lovren anaamini aliepushwa jambo hili ili acheze soka.

Mapenzi yake katika soka yalimfanya kuwa mtumwa Ujerumani kwani akiwa kijana mdogo ilimbidi kutumia dakika nyingi nje ha uwanja wa mazoezi wa Bayern Munich akiwasubiri nyota wa Bayern kipindi hicho kama Giovane Elber, Mario Basler na Bixente Lizarazu ili apige nao  picha, picha hizi za utotoni zilimfanya kuwa mshabiki wa Bayern Munich.
Dejan Lovren na familia yake hawakuwa na kibali cha kudumu Ujerumani, ilipofika mwaka 1999 waliambiwa waondoke nchini Ujerumani na ndipo walihamia Croatia ambako ndio asili ya mama yake na huko Lovren alifanikiwa kupata uraia wa nchi hiyo.
Maisha ya Croatia hayakuwa rahisi japo ndiko alianzia kucheza soka, Lovren anasema watu wa Croatia hawakuwa wanaamini katika kipaji chake akiwa mtoto na walimuambia hawezi kuwa mcheza soka mkubwa kwakuwa hakuwa na kasi na hajui kutumia mguu wa kushoto. 
Lovren anadai alikuwa na miaka 10 tu wakati akihamia Croatia na watoto wenzake walikuwa wakimcheka na kumbeza sana kwa kuwa hakua anajua kuongea lugha yao, na alikuwa akishindwa kucheza nao vizuri na hili lilimkomaza akaendelea kupambana.

Mitihani migumu katika soka lake ilikuwa kila siku na haikuwa ajabu kwa mashabiki wa Liverpool kumshambulia kocha wao Jurgen Klopp baada ya kumpa mkataba mpya Lovren kwani wengi walitamani aondoke, lakini wakati huu ambapo zimebaki siku 3 tu kwa fainali ya Champions League Liverpool wanakwenda wakimchukulia Lovren kama moja ya nguzo zao tegemezi.
Kilichomtokea siku za mwanzo akiwa Liverpool kupondwa na mashabiki haikuwa hadithi mpya kwake “niliposajiliwa Lyon kila mtu alihoji kwanini kanunuliwa £10m? Mashabiki waliponda na waandishi walinisema vibaya, kila nikicheza soka nikikosea tu kidogo baasi kesho utaona picha yangu kila gazeti, nilikosewa heshima”.

Lovren kwa sasa ana miaka 28 lakini anasema hakuna aliyeweza kumkatisha tamaa kwani miaka 16 iliyopita(akiwa na miaka 12 tu) aliandika katika meza yao ya nyumbani kwamba siku moja atakuja kuwa mlinzi bora kabisa duniani jambo ambalo limeanza kuonekana.
“Watu walikuwa wakinicheka na wakisema sitaweza lakini wakati nikiwa naanza anza tu kucheza soka niliandika chuni kwenye meza kwamba siku moja nitakuwa mlinzi tegemezi, maneno mabaya yamenitengeneza kuwa hivi nilivyo leo” anasema Lovren.

Dejan Lovren anasema aliandika hivyo chini ya meza ambayo alikuwa akifanyia homeworks za shuleni kwao katika apartments moja aliyokulia nchini Crotia, na anaamini hadi sasa watu wanaoishi katika apartments hiyo wanayaona maneno yake na anatamani kurudi kwenda kuinunua meza hiyo kwakuwa anaamini ni kitu muhimu kwake.
Lovren anakiri kuumizwa na kejeli pamoja na maneno ya kebehi ambayo mashabiki wa Liverpool walikuwa wakimtupia hapo mwanzoni, lakini muunganiko wake na Virgil Van Djik umefanya pacha yao kuiweka Liverpool mahali salama.

Lakini anauzungunziaje mchezo wao dhidi ya Real Madrid? Lovren alikuwepo katika kikosi cha Liverpool ambacho kilikula bao 3-0 pale Anfield kutoka kwa Madrid mwaka 2014 na wakati huo wakiwa huo kocha alikuwa Brendan Rodgers.
“Niko mimi na Handerson tu ndio tulikuwepo kipindi kile(2014), Madrid hawakucheza na kikosi hiki cha sasa, tumebadilika sana na kilicho sawa na wakati ule ni jina letu tu “Liverpool”, tuko tayari kumkabili yeyote yule duniani na nadhani hilo tulilionesha dhidi ya Manchester City”.

Na vipi kuhusu Cristiano Ronaldo ambaye anaonekana kutozuilika? “Tutamsimamisha, muda mwingine ntacheza naye one on one na muda mwingine tutaungana kama timu kumzuia lakini mimi binafsi niko tayari kwa ajili ya kumsimamisha”.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post