Neymar aondolewa uwanjani kwa machela Ufaransa
PSG walicheza dakika 10 za mwisho wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani
Mshambuliaji wa Paris St-Germain Neymar aliondolewa uwanjani kwa machela baada ya kuumia wakati wa mechi ya ligi kuu dhidi ya Marseille ambayo walishinda 3-0.
PSG walimaliza mechi hiyo wakiwa wachezaji 10 kwani walikuwa wametumia nafasi zao zote za kuwabadilisha wachezaji.
Jeraha hilo linatilia shaka kuhusu iwapo ataweza kucheza mechi ya hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid siku tisa zijazo.
Mshambuliaji huyo aliyenunuliwa £200m alionekana kuumia kwenye kifundo chake cha mguu akimkimbiza mchezaji Bouna Sarr. Alionekana kupinda kifundo chake cha mguu.
PSG walilaza Marseille kwa urahisi, Kylian Mbappe akifunga bao la kwanza naye Rolando akajifunga kutokana na pasi ya Neymar na kuwazawadi bao la pili.
Edinson Cavani naye alifunga la tatu kutoka kwa pasi nyingine ya Neymar.
Paris St-Germain, ambao wamo alama 14 kileleni mbele ya Monaco katika Ligue 1, watakuwa wenyeji wa Real Madrid Jumanne Machi 6.
Wana kibarua kigumu baada ya kulazwa 3-1 mechi ya kwanza.
Neymar amefunga mabao 29 katika mechi 30 tangu ahamie PSG kutoka Barcelona kwa uhamisho uliovunja rekodi ya dunia majira ya joto.