Leo februari 26, 2018 unachezwa mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kati ya Simba SC dhidi ya Mbao FC, mechi hiyo ambayo ni ya marudiano itachezwa jijini Dar es Salaam baada ya timu hizo kukutana Mwanza katika mchezo wa kwanza uliomalizika kwa sare ya kufungana 2-2.
Kuelekea mchezo huo, kocha wa Mbao FC Etiene Ndayiragije amezungumza kuhusiana na maandalizi ya mechi hiyo ambapo wadau wengi wa soka wanaamini itakuwa ngumu kutokana na mbao kuzisumbua vilivyo timu kubwa.
“Tunashukuru tumefika salama vijana wote wako sawa hakuna majeruhi yeyote, tulikuwa na tatizo kidogo la mchoko baada ya kutoka Njombe lakini tumefika tumepumzika naona vija wote wako katika hali nzuri kwa hiyo tunaimani mechi itakuwa nzuri.”
Etiene vs Simba kwa mara ya kwanza Dar
“Mimi sijawahi kucheza na Simba Dar, ni mechi yangu ya kwanza halafu kuna mabadiliko, kikosi sio kile cha msimu uliopita kwa hiyo hakuna uhusiano na mwaka jana. Tumejiandaa kwa ajili ya mechi ya msimu huu kwa hiyo tunasubiri kuona baraka za Mungu.”
Etiene haihofii Simba licha ya timu hiyo kucheza mechi 18 bila kupoteza, amesema Mbao ipo kwenye ligi kama ilivyo Simba na walikuwa wanatambua watakutana nayo.
“Simba ni timu ambayo ipo kwenye ligi na sisi tupo kwenye ligi kwa hiyo tulifahamu kama tutacheza na Simba, nikiangalia kikosi chao na kile tulichocheza nacho mwanza hakuna mabadiliko, wameongezeka wachache lakini timu ni ileile. Nimejiandaa na vijana wangu tayari wameshapata uzoefu kwa hiyo hakuna shida.”
Mbao imekuwa ikionesha soka zuri sana ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani CCM Kirumba, mwanza tofauti na inapocheza nje ya uwanja wake wa nyumbani, kocha amefafanua sababu ya kushindwa kucheza kwa kiwango kilekile pindi wawapo ugenini.
“Ukitoka nje ya uwanja wa nyumbani kuna mambo mengi huwa yanatokea kwa sababu kwanza kuna kusafiri kwa basi umbali mrefu, ugenini kuna kuwa na changamoto nyingi kama marefa na viwanja mara nyingi vinakuwa vinasumbua.”
Mbao imecheza mechi 18 na kukusanya pointi 19, ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi, kocha anazungumzia mwenendo wao msimu huu.
“Hatujaenda vibaya, timu bado ipo vizuri timu inaendelea kujiandaa kwa sababu wachezaji wengi walikuwa wapya lakini wanaimarika mechi hadi mechi na timu inaendelea kubadilika. Tutapambana na vijana wangu kuhakikisha tunaifikisha timu sehemu nzuri.”
“Timu nyingi zimejiandaa pia timu nyingi zimeiga kutumia vijana kwa hiyo ndio inasababisha kuwe na ugumu kwenye ligi lakini tatizo linaanza kuwa waamuzi.”