Klabu ya soka ya Barcelona imekanusha taarifa zinazosambaa mtandaoni kuwa imefikia makubaliano ya kumsajili nyota wa Atletico Madrid Antoine Griezmann.
Katika taarifa iliyotolewa mchana huu na Barcelona imeeleza kuwa klabu haihusiki wala haiungi mkono taarifa zinazoendelea kusambazwa kuhusu mchezaji huyo kufikia makubaliano ya kusaini mkataba na klabu hiyo.
''FC Barcelona haihusiki na habari ambayo imeanza kusambaa masaa machache yaliyopita katika vyombo vya habari tofauti kuhusu mchezaji wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann kuhususishwa na klabu yetu'', imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Mapema leo mitandao mbalimbali imeripoti kuwa nyota huyo wa Ufaransa mwenye miaka 26 amekubaliana mambo binafsi na klabu ya Barcelona hivyo kilichobaki ni pande mbili za klabu kukubaliana.
Aidha Barcelona inayoongoza msimamo wa La Liga ikiwa na alama 51 ikifuatiwa na Altetico Madrid yenye alama 42 imeeleza kuwa wao kama taasisi wanaiheshimu taasisi ya Atltico Madrid.