December 12 mwaka jana, 2017 wakati Rais John Magufuli akihutubia katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi CCM alieleza kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaofuatilia muziki kwa ukaribu ila kuna jambo ambalo linamkera.
Rais Magufuli alieleza kukerwa na baadhi ya wasanii ambao wanavaa nguo zisizo za maadili katika video za ngoma zao kitu ambacho kimefanya baadhi ya maadili kuanza kupotea.
“Kila ninapofungulia miziki ukitaka kuona wanaocheza utupu ni wanawake na wanaume hapana, wanacheza wakiwa wamevaa sana sana wataacha kifua wazi,” alisema.
Rais Magufuli alimaliza kwa kuitaka jumuiya hiyo kwenda kusimamami maadili katika maeneo ambayo wanatokea.
Mjadala katika Bongo Flava
Baada ya kauli ya Rais Magufuli mjadala ukawa mkubwa katika kiwanda cha muziki Bongo kutokana na baadhi ya video/wasanii kuonekana kuhukumiwa moja kwa moja na kauli hiyo.
Lakini kabla ya Rais Magufuli kuzungumzia hilo, msanii mkongwe wa Bongo Flava Afande Sele alikuwa ameshataja baadhi ya nyimbo pamoja na wasanii ambao alidai wamekuwa wakikiuka maadili.
Mkali huyo wa rhymes alitaja ngoma kama Wowowo ya rapper ZaiiD, Mwanaume Mashine ya Msaga Sumu huku akieleza kukerwa na tabia ya msanii na video vixen, Gigy Money ambayo alidai anapenda kuvaa nusu utupu.
“Gigy Money namsikiaga kuwa ni dada ambaye anapenda kukaa uchi, anapenda kufanya vitu sijui vya aina gani huo ndio mmomonyoko wa maadili, hivyo inaonekana malezi yake hayana maadili,” Afande aliiambia East Africa Radio.
“Kuna vitu vingi anavifanya vinafanya ajulikane kabla ya huo muziki alikuwa anajulikana kwa kumwaga radhi,” aliongeza.
Hata hivyo siku iliyofuata Gigy Money ajibu tuhuma hizo kupitia mtandao wa Instagram kwa kueleza kuwa wasanii wa zamani wamuache na kuonekana kupuuzia jambo hilo.
Muda ni Jawabu
Muda ni kikokotoa ambacho hutua majibu ya maswali magumu ambayo yameshindikana kwa kipindi fulani.
Baada ya suala la Afande na Gigy kupita, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliwaita Gigy Money na Mwanamitindo Sanchoka kwa mahojiano maalumu kuhusu kazi zao ambazo zinaonekana zipo kinyume na maadili.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza alitamka Gigy mbele ya waandishi kuripoti ofisi kwake kutokana na kosa la picha za uchi.
Hata hivyo baada ya kufika Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) aliambiwa haijaitwa hapo ila anatakiwa kumtafuta waziri ili kujua nini alichokifanya na sasa bado suala hilo linaendelea.
Twende pole pole, si Afande Sele pekee ambaye aliwahi kukemea hilo, pia si Gigy Money na na Mwanamitindo Sanchoka ambao wanakiuka maadili.
Maoni ya Ma-director Bongo
Ma-director wa video za muziki Bongo walipata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu agizo la Rais Magufuli na hatua zinazochukuliwa, miongozi mwao ni Nicklass na Nisher walipohojiwa na EATV.
Nisher: Kauli ya Rais ni sheria hatuwezi kuipinga, kuna upande kitabadilisha kidogo, kwa upande wa picha kwenye runinga zetu isipokuwa ni kitu lazima kifanyike.
So siwezi kupingana na kauli ya Rais ni vitu ambavyo tunatakiwa tuwe wabanifu zaidi, kujua tunafanya kitu kiwe na muonekano tofauti na kiweze kuuza.
Nicklass: Lazima maadili yetu ya nchi yalindwe tusije baadaye tukabomoka kwa sababu tunaenda taratibu mwisho wa siku tukajikuta nje ya mchezo kabisa, so inabidi wakubwa wetu kama hivi wakumbushe.
Kikubwa nikusikiliza ambacho tunatakiwa kukifamya kwa sababu hatujaonewa na video sio lazima uonyeshe ‘vyupi’, ni ubunifu kwanza, wape watu stori kali mwisho siku video itapendwa sio lazima uonyeshe maungo ndio video ipendwe.
Kwa Maslai Mapana
John T. Molly mtungaji wa kitabu cha Dress for Success anasema kuwa jinsi tunavyovaa huongeza sana maoni ya watu ambao tunakutana nao kila siku kitu ambacho kwa kiasi fulani huathiri jinsi wanavyotutendea.
Tukirejea katika stori ya Gigy Money awali alipoitwa Basata alilalamika kuwa hatua zilizoanza kuchukuliwa dhidi yake zililenga kumuonea kwa sababu picha zisizoa za maadili alishaacha kupiga.
Hata hivyo kwa mujibu wa Dress for Success hatua zilizochukuliwa na zitakazokuja kuchukuliwa hapaswi kulalamika kwani mazingira aliyatengeneza mwenyewe katika hilo.
Dkt. James P. Comer anasema kila mtu amekifanya kizuri kwa wakati wake na jinsi unavyoonekana yaweza kuwa na tokeo kubwa juu wengine wanavyokuona na kukutendea.
Uwepo wa video zisizo na maadili katika runinga zetu hufanya baadhi ya watu hasa watoto kusadiki kuwa ndivyo maisha yalivyo. Vijana walio katika rika la balehe ni waanga wakubwa wa hilo.
Hali ilivyo ni kwamba kwenye runinga, magazeti na majarida wanaume na wanawake wenye hukodolewa sana macho (kuvutia), mara nyingi vijana hushindwa kuelewa kwamba warembo wa kwenye runinga na magazetini hupambwa na timu ya warembeshaji.
Mkurungezi wa Career Development, Vicki L. Baum anasema wanawake wengi huvurugika akilini waendapo katika mahojiano ya kupata kazi, hufikiri ni kama kufanya matembezi na wapenzi wao.
Anaendelea kwa kueleza kuwa muda mwingine huhisi kama wanatongozwa na matokeo yake hujikuta wakipoteza kazi ambazo walikuwa wakitazamia kuzipata.
Hii yote hujengwa na vile wanavyotazama kwenye runinga, mitandao na kusoma kwenye magazeti. Hivyo sote tukuliane ili kuepusha hilo hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa bila kuathiri pande zote mbili.