LICHA ya kutokiri moja kwa moja juu ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu kumkamata Askofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGFC) lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limesema ni lazima litamhoji kiongozi huyo wa kiroho.
Kuhojiwa huko kumetokana na kauli yake dhidi ya serikali aliyoitoa wakati wa ibada ya Krismasi.
Jana, kulienea taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kueleza kwamba askofu huyo alitiwa mbaroni jana asubuhi na askari wa Jeshi la Polisi huku sababu za kukamatwa zikielezwa kuwa ni ujumbe alioutoa wakati wa mahubiri yake ya ibada ya Krismasi.
Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na ukweli wa taarifa za kutiwa mbaroni kwa Askofu Kakobe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa ni kweli walishakuwa katika harakati za kumkamata
.
"Ametoa maneno ya kashfa katika mahubiri yake, lakini sina taarifa kama amekamatwa," Kamanda Mambosasa alisema na kuongeza:
"Taarifa za kumkamata zipo, lazima tumkamate. Tutamhoji…tutamhoji alikuwa na maana gani.“Mtu akitenda kosa la jinai ni lazima akamatwe…kwa sasa niko msibani, sijapokea taarifa kama amekamatwa au kuhojiwa. Nitawaarifu kama kutakuwa na taarifa zaidi.”
Hata hivyo, hadi Nipashe ikienda mitamboni hakukuwa na taarifa zozote rasmi kuhusiana na kukamatwa kwa Kakobe.
Awali, Nipashe ilimuuliza Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Muliro, ambaye pia alidai hakuwa na taarifa za kukamatwa kwa askofu huyo.
Askofu Kakobe (62), anadaiwa kuyatumia mahubiri yake siku hiyo kuzungumzia mwenendo wa serikali na masuala mbalimbali ya kisiasa nchini.
Mojawapo ya sauti inayodaiwa kuwa ya Askofu Kakobe na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ilidai kwamba hivi sasa Tanzania si nchi ya chama kimoja kama viongozi wanavyotaka.
Jana jioni, Nipashe ilifika katika kanisa la Kakobe, Mwenge na kukuta shughuli za kila siku kanisani hapo zikiendelea kama kawaida huku baadhi ya waumini waliokuwapo wakisema hawakuwa na taarifa za kutiwa mbaroni kwa kiongozi wao huyo.
Chanzo: Nipashe
Tags
kitaifa