BAADA ya kuenea taarifa kwamba mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere yupo mbioni kutimka klabuni hapo, wakala wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba, ameibuka na kufungukia hatma ya mteja wake huyo.
Kagere aliyejiunga Simba msimu wa 2018/19 akitokea Gor Mahia ya Kenya, msimu wa 2020/21 uliomalizika hivi karibuni, alikosa nafasi kubwa ya kucheza kutokana na ushindani wa namba alioupata mbele ya John Bocco na Chris Mugalu.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka nchini Ukraine, wakala huyo alisema: “Tayari Meddie ameongeza mkataba na ataendelea kubaki ndani ya Simba, hivyo watanzania wasitegemee kuwa ataenda kujiunga na klabu nyingine.
“Watu wataendelea kumuona Simba kwani wamemuongezea mkataba japo kwa sasa klabu imeweka maficho sana ila wataliweka wazi baadaye,".
Hivi karibuni ilielezwa kwamba, Kagere aliandika barua ya kuomba kuondoka Simba, huku akihusishwa kutakiwa na timu nyingine nje ya Bongo.