Na Thabit Madai, Zanzibar.
Wanaharakati wanaopiga vita Vitendo vya udhalilishaji kwa watoto visiwani Zanzibar, wamesema kwamba ukosefu wa Elimu ya ndoa kwa wanandoa, ndio chanzo kikubwa kwa ndoa nyingi kuvunjika na kupelekea kushamiri kwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto pamoja na kuongezeka kwa watoto wa mitaani.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati ya kupambana na vitendo vya udhalilishai kutoka Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ( JUMAZA) , Sheikh Ali Abdallah Amour wakati akizungumza na Mwanishi wetu, katika mradi wa kutetea haki za watoto unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulukia watoto Duniani UNICEF,
Mradi huo unatekelzwa kwa karibu na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)
Sheikh Ali Abdallah Amour alisema kuwa wanandoa wengi katika miaka ya hivi karibuni, hawajuwi hasa elimu ya ndoa, hali inayopelekea ndoa hizo kuvunjika na kuongezeka watoto mitaani pamoja na kushamiri kwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya Udhalilishaji.
Alisema kuwa katika tafiti zao nyingi ambazo wamefanya wamebaini kuwa baadhi ya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto husababshwa na wazazi kuachana.
“Tulipopita katika jamii tumegundua kuwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto husababishwa na wazazi wengi kuachana” alisema Sheikh Amour.
Alifahamisha kuwa kama wazazi wanapoachana bila shaka hawakuwa na elimu ya ndoa ndo maana wameachana na kupelekea watoto wao kuhangaika hadi kufikia kudhalilishwa.
“Ili kumaliza suala zima la udhlilishaji kwa watoto Nchini lazima wazazi wawe na elimu ya ndoa ambapo Talaka zisizokuwa na msingi zitaepukika na watoto kulelewa na wazazi wao jambo litakalopekea kupunguza vitendo hivyo” alieleza Sheikh huyo.
Hata hivyo alifahamisha kwamba Jumuiya ya Maimamu Zanzibar imekuja na suluhisho la jambo hilo kwa kuanzisha vyuo vya ndoa ili kuwafundisha wanandoa pamoja na wanandoa watarajiwa thamani ya ndoa na mambo ya kuzingatia katika kutunza ndoa zao.
“Katika chuo hicho tunawafundisha Ndoa ni nin,Thamani ya ndoa pamoja na ubaya wa Talaka kwa ujumla” alifahamisha.
“hata hivyo katika vyuo hivi tunajaribu kuwafamisha suala zima la malezi maana tumepokea baadhi ya kesi kuwa baba amembaka mtoto wa mkewe na kesi nyngine nyingi” aliongeza kufahamisha.
Alisema wao wanaamini kuwa jamii itakapo endelea kuitikia kwa wingi katika vyuo hivyo itapelekea kupunguza Suala la udhalilishaji kutokana na masomo wanayofundishwa huko.
Katika hatua nyingine alisema kuwa kwa kipindi kifupi tangu kuanza vyuo hivyo imeonesha kwa kiasi kikubwa ufanikiwa kupunguza kesi za udhalilishaji kwa watoto pamoja na kesi za talaka.
“Hapo awali kule kwa kadhi kulikuwa na mafuriko ya watu wanaleta madai juu ya kutaka kuachana kwaasa baadhi yao kupata elimu ya ndoa kesi nyingi zimepungua kupelekwa na wengine hufikia hatua za kuzishuluhisha wenyewe majumbani na wazee wao” alisema Sheikh huyo.
Kwa Upande wake Bi Halima Kassimu Mohamed mwanaharakati wa kutetea haki za watoto visiwani hapa anaeleza kuwa kuongezeka kwa ndoa nyingi kuvunjik pamoja na kukithiri kwa kesi nyinyi za watoto kudhalilishwa inatokana kuwa jamii imeacha kuishiii kwa mujibu wa dini na tamaduni zao.
“Hapo nyuma suala la malezi halikuwa hivi tulikuwa tunaishi kwa kufuata msingi ya Dini pamoja na kufuata mila na tamaduni zetu, ilikuwa mtoto wa mwenzio basi na wewe ni wak ukimkuta amekosea unamkanya ila kwa sasa imekuwa kinyume kabisa” alieleza.
“hali hiyo ndo imetufikisha hapa Talaka zinatolewa kila siku, watu wanaingia katika ndoa wakiwa hawajui elimu ya ndoa na hawajui wapi pa kuipata ndo maana kila kitu kinakuja” alieleza Bi Halima Kassimu Mohamed.
Tags
MAHUSIANO