Lamine Moro Ampa Ulaji Beki Mrundi Yanga SC

Beki wa Yanga, Lamine Moro.
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umesitisha mipango ya kuachana na beki wa kati wa kimataifa wa timu hiyo Mrundi Moustafa Selemani na badala yake ataendelea kukipiga kwenye klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam.

Beki huyo ni miongoni mwa wachezaji wa kimataifa waliokuwa wanatajwa kuachwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo unaotarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu.

Yanga tayari imetangaza kuachana na wachezaji wake wa kimataifa watatu ambao ni Mganda Juma Balinya, Mzambia Mybin Kalengo na Mrundi Issa Bigirimana ambao wote walisajiliwa kwenye usajili wa msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Moustafa ataendelea kubakia kuichezea Yanga baada ya kutojua hatma ya Lamine aliyeandika barua ya kusitisha mkataba huku viongozi wakipambana kumbakisha kikosini.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kama uongozi ungekuwa na uhakika wa kurejea kwa Lamine aliyerudi nyumbani kwao Ghana, basi wangeachana naye lakini kutokana na sintofahamu iliyokuwepo kati ya beki huyo na uongozi, basi wanasubiri kuona nini kitatokea.

Aliongeza kuwa beki huyo hivi sasa anaandaliwa kucheza pamoja na beki mkongwe Kelvin Yondani baada ya Lamine kutoeleweka hatma yake kama anarejea Yanga au anabaki nyumbani kwao.

“Ni ngumu kumuacha Moustafa katika kipindi hiki ambacho tayari beki wetu tegemeo aliyekuwa akicheza pamoja na Yondani kutojua hatma yake anarejea Yanga au anaendelea kubaki kwao Ghana baada ya kusitisha mkataba wake,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla alisema: “Uongozi wetu umepanga kufanya usajili mzuri wa kisasa na ndiyo sababu utaona tumeachana na wachezaji wa kimataifa ambao wameonekana kwet u hawana msaada akiwemo Sadney (Urikho) na Balinya (Juma).”
STO

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post