Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Tanzania(IGP) Simon Sirro amesema uchunguzi juu ya kupotea kwa mwandishi wa habari za Uchunguzi Azory Gwanda wa gazeti la mwananchi unaendelea kwani wameshafungua jalada la uchunguzi, huku akiwataka watu kama wana taarifa kuhusu tukio hilo kuzifikisha polisi na si kuishia mitandaoni kwani haziwezi kusaidia.
Akizungumza katika kipindi maalum cha Konani kinachorushwa na ITV kupitia Mitandao yake ya Youtube na Facebook, IGP Sirro amesema suala la watu kupotea halijaanza leo huku akitolea mfano wa wazee wa kizanaki wengi walikuwa wanasemekna wamepotea lakini baadae wanaonekana.
Katika hatua nyingine IGP Sirro amezungumzia suala la aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu kupigwa risasi ambapo amesema mpaka sasa bado hawajambaini mtu aliyefanya tukio hilo, huku akieleza kwamba Tundu Lissu ameshindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo jambo ambalo linachukua muda.
"Sisi tunamsubiri Mhe.Tundu Lissu aje afungue kesi, kitu gani kimemtokea, mazingira gani na yule dereva wake, dereva tumemtafuta imekuwa shida, yeye mwenyewe alipopata matatizo yupo nje hatujamuona, tunamuona tu kwenye mitandao"IGP Sirro.
IGP Sirro ameweka bayana kwamba kesi ya jinai mara nyingi haifi hata ikichukua miaka kumi bado ni kesi ya jinai, "Kimsingi ni kwamba kesi ipo tunamsubiri Bwana Lissu aje atupe taarifa ilikuwaje na yule shahidi yake nafikiri tutapata sehemu ya kuanzia.
Tags
HOT NEWS