MWANAMAMA kunako Bongo Fleva, Mwanahawa Abdul Jumaa almaarufu Queen Darleen ambaye ni dada wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amepasua jipu.
AFICHUA SIRI
Queen Darleen amefichua siri ya kaka’ke huyo kutomuoa mwandani wake wa sasa, Tanasha Donna Oketch ambaye amemzalia mtoto wa kiume hivi karibuni aitwaye Nasibu Junior.
Queen Darleen ambaye ‘ameshea’ baba na Diamond au Mondi, ameliambia gazeti hili kuwa, jamaa huyo hajamuoa Tanasha kwa sababu anahofia kwamba atapungukiwa na vitu fulanifulani ikiwemo kupoteza mashabiki wanawake ambao ni wengi.
AHOFIA KUBANWA
Queen Darleen alisema kuwa, Mondi anahofia mno kuoa na akisema tu amuoe Tanasha, basi atashindwa kufanya mambo mengi kwani atabanwa na ndoa. Hata hivyo, Queen Darleen hakufafanua ni mambo yapi hayo ambayo Mondi atashindwa kuyafanya.
Kwa mujibu wa Queen Darleen ambaye amemtangulia Mondi kuzaliwa kwa baba yake, Mondi hataki kuoa mapema, lakini pia hataki kumvunja moyo Tanasha ambaye humuambii kitu kutokana na jinsi alivyokufa na kuoza kwa Mondi. Mwanamama huyo alisema, mara nyingi Mondi huwa ni muwazi kwani husema waziwazi kuwa hayuko tayari kwa ajili ya ndoa kwa sasa.
ANATAKA NDOA ZA MITARA
Queen aliendelea kusema kuwa, Mondi hupendelea mno awe kwenye ndoa za mitara (yaani aoe mwanamke zaidi ya mmoja) na hiyo ni kwa sababu mojawapo inayomfanya alegeze kamba katika kufanya uamuzi wa kuoa kwa sasa.
“Sisi hujadiliana sana kuhusu masuala ya ndoa, (Mondi) ni mtu anayehofia sana kujiingiza kwenye ndoa.
“Anataka ajiandae ipasavyo kabla ya kuamua kufunga pingu za maisha,” alisema Queen Darleen ambaye ni mmoja wa wasanii walio chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na Mondi.
QUEEN DARLEEN AUNGANA NA MAKONDA
Kauli hiyo ya Queen Darleen inakuja miezi kadhaa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda naye kumwambia Mondi asioe kwanza, badala yake aendelee kuongeza familia ya Wasafi.
Makonda alimpa Mondi ridhaa ya kutokuoa na kumtaka aendelee kuwa ‘sukari ya warembo’ kwa jinsi anavyojitoa kusaidia watu mbalimbali kwenye jamii.
Makonda ambaye ni mlezi wa Wasafi alisema kwa kazi anayofanya Mondi huenda akioa mapema itamletea shida na kwamba anahitaji muda zaidi wa kufikiria kuwasaidia Watanzania wenzake.
“Haya mambo mkiyajua vizuri bana…kwanza ukiwa msanii, halafu mashabiki wako wengi wakiwa wanawake, ukioa wanaweza kukukimbia, utafikiri ungewaoa wote,” alisema Makonda.
DANADANA ZA MONDI KUMUOA TANASHA
Kuhusu kumuoa Tanasha, mapema mwaka jana, Mondi aliahidi kufanya hivyo Februari 14 (Siku ya Wapendanao), lakini hakufanya hivyo kwa kile kilichoelezwa kwamba, anajua akioa atapoteza mashabiki wake wengi ambao ni wanawake.
ALIFANYA HIVYO KWA ‘MAEKSI’ WAKE
Kinachomtokea Tanasha kinaelezwa kuwakuta waliokuwa wapenzi wa Mondi (maeksi) ambao nao aliwapiga danadana kisha kuzaa na kutengana naye.
Mashabiki wengi wa Mondi waliamini angemuoa mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye alizaa naye watoto wawili, lakini Zari aliambulia patupu kama ilivyokuwa kwa Wema Sepetu, Hamisa Mobeto na wengineo.
NEEMA ADRIAN, RISASI
Tags
CELEBRITY