Hisia 8 za kuepuka katika mapenzi



MIONGONI mwa vitu vinavyochangia kuharibu uhusiano wa kimapenzi ni hisia mbaya. Wapenzi wengi wameachana kwa sababu si kwamba walithibitisha ubaya wa wenza ila walijijaza wenyewe hisia mbaya na kujikuta wamepoteza hisia za kupenda. Zifuatazo ni hisia nane hatari ambazo unatakiwa kuepukana nazo
NASALITIWA
Kuishi katika mapenzi huku ukiwa na fikra kwamba mwenza wako anakusaliti ni jambo baya kwa vile huathiri msukumo wa ndani wa kupenda. Matokeo yake utajikuta ukishindwa kutimiza wajibu wako kama mke/mume kwa sababu tu ya kuendekeza hisia mbaya.
TUTAACHANA
Kuna wapenzi ambao wanaishi na mawazo ya “ipo siku tutaachana”. Wanafanya hivyo eti kwa kutafsiri mwenendo usioridhisha wa mapenzi yao. Kusema kweli hili ni jambo baya kwani huondoa ari na kujenga ufa wa mapenzi.
Huwafanya wapenzi kubakia na wazo moja tu la kutafuta sehemu mbadala ya kwenda baada ya kuachana. Usiwaze kabisa kuachana hata kama mnagombana.
SIWEZI FARAGHA
Baadhi ya wapenzi huwa na hisia kwamba si wajuzi kwenye sita sita. Hata kama hawajaambi­wa chochote kuhusu kuto­watosheleza wenza wao faragha hukimbilia kujihukumu. Hujaam­biwa kama umecheza chini ya kiwango, hofu ya nini? Usi­waze hivyo!
NINA KASORO
Naamini mitaani wapo watu ambao huamini wana kasoro fulani ndiyo maana hawafikii viwango vya kupendwa kama wanavyovihitaji. “Yaani mimi ningekuwa kama fulani ningefurahi sana.” Epuka kujishusha hadhi kwenye hisia zako.
NITAMUUA
Miongoni mwa hisia mbaya kabisa kwenye mapenzi ni kufikiria kumu­ua mwenzako kwa sababu yoyote. “Nikimfu­mania na mwanaume mwingine nitamuua.” Mtu anaye-tawaliwa na mawazo ya aina hii anajiweka katika mtego mbaya kisaikolojia wa kuja kutekeleza kile anachojiapiza hata kwa sababu ndogo. Usifikirie hivyo maishani mwako.
NIMEKOSEA KUCHAGUA
Usijihukumu makosa kwa sababu umeona mpenzi wako ana tatizo fulani. Fahamu kuwa kasoro ni sehemu ya ubinadamu. Weka mikakati ya kumuongoza mwezio kuliko kuhitimisha kwa mawazo kwamba ulikosea kumchagua.
HATUWEZI KUZAA
Kuna wapenzi ambao kwa kuishi miaka mitatu au minne pamoja bila kupata mtoto hufikia kwenye fikra kwamba hawawezi kuzaa. “Mmm, mwaka wa nne umepita bila mtoto, nadhani sisi hatuwezi kuzaa.”
Kwa nini msizae? Hizo ni fikra zako, hamjaambiwa na daktari sasa iweje uwaze hivyo? Jipe moyo kwani kuna watu walizaa baada ya miaka kumi, iweje ninyi wa mwaka mmoja?
ANANIDANGANYA
Ipo aina ya watu ambao hata kama wakiambiwa wanapendwa sana, hukimbilia kusema na kuamini kuwa wanadanganywa. “Mmm unanidanganya.” Atasema hivyo licha ya kuona mwanaume/ mwanamke anavyowajibika kwake. Hili ni jambo baya, ukioneshwa mapenzi usihisi acha kuhisi kuwa unadanganywa.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post