ZAHERA APATA MBADALA WA MSUVA YANGA

YANGA hawana raha tangu auzwe winga wao matata, Simon Msuva kwa klabu ya Difaa el Jadida ya Morocco. Lakini sasa Kocha Mwinyi Zahera anawaletea sapraizi mashabiki wa klabu hiyo.



Habari zinasema kwamba Zahera yuko kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na Winga machachari wa Kariobangi Sharks, Harrison Mwendwa ( aliyebebwa).



Mchezaji huyo anayesifika kwenye Ligi Kuu ya Kenya ana uwezo wa kucheza winga ya kushoto na kulia na aliwalaza mabeki wa Yanga na viatu walipokutana kwenye michuano ya SportPesa Jijini Dar es Salaam.



Yanga imekuwa na shida ya viungo washambuliaji wa pembeni (winga) tangu kikosi hicho kilipomuuza Simon Msuva ambapo walijaribu kumrejesha Mrisho Ngassa lakini Zahera hajamuelewa.




Habari zinasema kwamba Zahera amemuelewa sana Harrison ambaye anaamini kwamba atamaliza tatizo lililopo kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga kwani Heritier Makambo hana wa kumlisha mipira kwa vile anawazidi kasi wachezaji wengi.



Kama dili hiyo itamalizika vizuri huyo atakuwa ni mchezaji wa Yanga kumng’oa Sharks kwani tayari imeshakubaliana na Duke Abuya ambaye ni mshambuliaji kilichobaki ni kusaini tu.



Viongozi wa Sharks waliiambia Spoti Xtra jana kwamba wanajua kuna wachezaji wao wanatakiwa na Yanga akiwemo Duke na Harrison lakini wanaisubiri Yanga mezani. Mbali na hao wawili pia Zahera ameshakubaliana na straika Mzimbabwe, anayeichezea FC Lupopo, Rodrick Mutuma ambaye inaripotiwa tayari amefichwa Dar es Salaam na anaendelea na mazungumzo na ishu itamalizwa kimyakimya.



Mwingine ambaye ameshachukua mpaka advansi kitambo ni kipa namba moja wa Bandari FC ya Mombasa, Farouk Shikala ambaye Kocha wake, Ben Mwalala amemtaja kama kipa namba moja wa Kenya kwa sasa.



Dili pekee ambayo bado inamuumiza kichwa Zahera ni straika wa Gor Mahia ya Kenya, Jacques Tuyisenge ambaye bado hawajakubaliana dau kwa vile wakala wake anataka dau kubwa na inaelezwa kuwa siku chache zijazo atasaini mkataba kwenye kikosi cha AS Vita kwa dau la dola 190,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 400.



“Tayari tumemalizana na winga mwingine ambaye atakuja kumaliza tatizo la eneo hilo ambalo kwa msimu huu limekuwa likitusumbua.



“Tumemchukua Mwendwa ambaye yeye ana uwezo mkubwa wa kucheza nafasi hiyo ya winga, na matarajio ya kocha Zahera ni kuona yeye akimaliza tatizo la winga ambalo linatusumbua baada ya kuondoka kwa Msuva,” kilisema chanzo hicho.



Msimu wa Ligi Kuu Bara unamalizika Mei 28 huku ikielezwa kwamba lengo la Zahera ni kumaliza usajili mapema kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon kwani atakuwa bize na DR Congo kama Kocha Msaidizi

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post