YONDANI ALETEWA MSAIDIZI YANGA



YANGA wanafanya mambo yao kwa siri kubwa huku wakipania kuwapa bonge la sapraizi mashabiki wao kwenye usajili wa safari hii. Lakini Spoti Xtra limebaini kwamba wako kwenye mazungumzo na beki wa kati wa Polisi FC ya Rwanda, Aimable Nsabimana.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera na baadhi ya vigogo wa Jangwani ndio wanaendelea na mazungumzo na wakala wa mchezaji huyo na Spoti Xtra limethibitisha kuwa dili litamalizika haraka kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon Mwezi Juni.

Zahera amewaambia Yanga kwamba anataka kukamilisha kila kitu kabla ya kujiunga na DR Congo kwenye kambi ya Afcon kwani atakuwa bize sana. Tayari Yanga wameshamaliza kwa siri na kipa wa Bandari ya Kenya, Farouk Shikalo kuchukua nafasi ya Klaus Kindoki ambae ataachwa baada ya msimu kumalizika kutokana na kiwango duni ambacho hakiendani na Sh. Mil 6 anazokinga.

Taarifa ambazo Spoti Xtra imezipata jana ni kwamba beki huyo mwenye mwili mkubwa, anatakiwa na Yanga ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo ina watu kama Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Andrew Vincent ‘Dante’ ambao wanaonekana kuzidiwa na majukumu.

Mbali na Yanga pia habari zinasema Zesco ya Zambia inamuhitaji pia beki huyo raia wa Rwanda mwenye uzoefu mkubwa na asiyesumbuliwa na majeruhi. Meneja wa mchezaji huyo ambaye pia ni meneja wa Meddie Kagere wa Simba, Patrick Gakumba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, Nsabimana mwenye uwezo wa kucheza beki wa kati namba nne na tano, anahitajika kwa nguvu sana na Yanga.

“Huyo beki Yanga wanamtaka sana, sio wao peke yao, bali hata na Zesco. Ana uwezo wa kucheza beki wa kati, yaani namba nne na tano. “Wanatuma mtu aje huku Rwanda nizungumze nae, tumalize kuhusu usajili wa mchezaji huyo, nawasubiri,” alisema Gakumba ambaye pia anaendelea na mazungumzo na Yanga juu ya usajili wa mteja wake,straika wa Gormahia Jacques Tuyisenge.

Nsabimana kwa sasa yupo Police FC aliyojiunga nayo Februari, mwaka huu kwa mkataba wa miezi sita akitokea Becamex Bình Dưưng FC ya Vietnam. Kumbukumbu za Nsabimana zinaonyesha amecheza APR ya Rwanda tangu 2016 mpaka 2018 enzi hizo akivaa jezi namba 50, amezaliwa mwaka 1997.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post