Marekani inabeba dhima ya chinja chinja ya Saudia


Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah imelaani vikali kitendo cha utawala wa Aal-Saud cha kutekeleza hukumu ya kuwanyonga makumi ya Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia na kusisitiza kuwa, jinai hizo za kihaini zilifanyika kwa baraka kamili na ushirikiano wa Marekani.

Taarifa ya harakati hiyo ya muqawama ya Hizbullah imebainisha kuwa, "Marekani ndiyo mshirika mkubwa wa Saudia katika jinai zake. Marekani inapaswa kubebeshwa dhima kwa kuwa ndiye mtetezi na mlinzi wa utawala huo wa kifalme, na imekuwa ikiisukuma jamii ya kimataifa ishabikie jinai hizo za Saudia, kwa lengo la kulinda maslahi yake na fedha na mafuta."

Aidha taarifa hiyo ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah imekosoa vikali kimya cha dunia, mkabala wa jinai hizo za kutisha za Saudia inayokingiwa kifua na Marekani.

Jamii ya kimataifa imeendelea kulaani kitendo hicho cha watawala wa Aal-Saud cha kuwanyonga kwa kuwakata vichwa watu 37, aghalabu yao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na kisha kuanika mwili wa mmoja wa Waislamu hao waliowafanyia ukatili huo hadharani kwa ajili ya kutazamwa na umati.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International sambamba na kulaani hatua hiyo ya watawala wa Riyadh ya kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi kuwanyonga kwa umati Waislamu wa Kishia, limesisitiza kuwa utawala huo wa kifalme hauheshimu thamani ya utu.

Kadhalika Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa ameonyesha wasi wasi wake mkubwa juu ya kukosekana hali ya uadilifu katika vyombo vya mahakama nchini Saudia, hasa kutokana na ripoti zinazoeleza kwamba 'wahanga hao walikiri makosa yao chini ya mateso makali.'

    

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post