Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa halitaweza kuongeza muda wa usajili pale muda utakapofikia kikomo kesho Julai 26 2018.
Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Clifford Mario Ndimbo, amesema klabu zote kuanzia ngazi ya Ligi Daraja la Pili, Kwanza na Ligi Kuu zinapaswa kukamilisha usajili wao kupitia mfumo mpya wa TFF FIFA CONNECT.
Ndimbo amesisitiza klabu zote kufanya hivyo kabla ya saa 6 na dakika 59 kesho ambapo dirisha hilo litafungwa na zaidi ya hapo hakutakuwa na msalia mtume juu ya kuongezwa kwa siku za usajili.
Aidha, Ndimbo ameeleza kuwa klabu zote ambazo hazitakamilisha usajili baada ya tarehe 26 hazitaruhusiwa kushiriki ligi kuanzia msimu ujao.
Mpaka sasa klabu ambazo hazijakamilisha usajili wake ni pamoja na Ruvu Shooting, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Alliance, Mwadui FC, Kagera Sugar, Lipuli, African Lyon, KMC na Azam FC.
Ligi Kuu Bara inataraji kuanza kutimua vumbi mnamo Agosti 22 ambapo jumla ya timu 20 kutoka 16 msimu uliopita zitashiriki.