TFF:Kwa Uamuzi Huu wa Yanga Itapata Tabu Sana


WAKATI mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati "Kombe la Kagame" yanaanza leo jijini Dar es Salaam, bado Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) "linaponda" uamuzi wa kujitoa katika michuano hiyo uliofanywa na klabu ya Yanga, imeelezwa.

Yanga ilitangaza kujitoa katika mashindano hayo ikidai inajiandaa na mechi yake ya hatua ya makundi dhidi ya Gor Mahia itakayofanyika Kenya Julai 18 mwaka huu.

Akizungumza jana jijini, Kaimu Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani alisema kuwa uamuzi wa Yanga kujitoa haukulenga kuiimarisha timu yao kiufundi na hivyo imejiweka kwenye nafasi isiyo sahihi kuelekea michezo yao ya Kombe la Shirikisho.

Nyamlani alisema kuwa Yanga itakuwa na wakati mgumu kukabiliana na Gor Mahia pamoja na Rayon Sports ambazo zinashiriki michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Alisema huwezi kuwa kwenye ushindani kwa kucheza na mpinzani aliyetoka katika mashindano na wewe wachezaji wao wametoka nyumbani "kwenye likizo" ya mwezi mzima.

"Uwezo wetu wa kufikiri ni mdogo, haiwezekani kuna mashindano ya kukusaidia, unayakataa, huwezi kukutana na Gor Mahia kwa kufanya mazoezi ya wiki moja huku wachezaji wakitokea nyumbani, mpira una matokeo ya kikatili, tutarajie kupokea matokeo ya kikatili,"  alisema Nyamlani.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema jana kuwa maandalizi ya michuano hiyo itakayoshirikisha timu 12 yamekamilika na waamuzi wote 18 kutoka katika nchi wanachama walioteuliwa kuchezesha wamefaulu mtihani wa utimamu.

Musonye alisema kuwa zawadi za fedha ambazo jumla yake ni Dola za Marekani 60,000 zipo na kuwataka mashabiki wa soka wa Dar es Salaam na mikoa jirani kujitokeza kushuhudia michuano hiyo huku akiweka wazi ratiba haiingiliani na mechi za Kombe la Dunia.

Alisema leo katika mechi za ufunguzi kutakuwa na mechi tatu ambazo ni kati ya JKU kutoka Zanzibar dhidi ya Vipers ya Uganda wakati Azam watawakaribisha Kator ya Sudan Kusini na APR ya Rwanda itaivaa Singida United kuanzia saa 1:00 kwenye Uwanja wa Taifa.

Azam FC ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo yaliyofanyika kwa mara ya mwisho mwala 2015. 

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post