Leo tunazianza siku 4 za mitanange 8 ya hatua ya 16 bora ya Kombe la dunia.
Michezo inayotufungulia siku ya leo itatupa Burudani ya kuwaangalia wachezaji bora kabisa wa kizazi hiki-Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wakitetea bendera za mataifa yao.
Saa 11 jioni Lionel Messi ataiongoza Argentina kuumana na Ufaransa kwenye mchezo utakaochezwa katika dimba la Kazan Arena.
Saa 3 usiku itakuwa zamu ya Ronaldo kuiongoza Ureno kuumana na timu ambayo mpaka sasa haijaruhusu goli hata moja katika michuano hii-Uruguay .
Endapo Portugal na Argentina zitashinda mechi za leo basi tutashuhudia mpambano wa kwanza wa Messi vs Ronaldo katika robo fainali siku ya Alhamisi.
Kuelekea game hizi za 16 bora Ufaransa vs Argentina na Uruguay vs Portugal Shaffih Dauda amewapiga chini kina Pogba na Ufaransa yao, mkeka wake amewapa Argentina licha ya kuungaunga hatua ya makundi bado anaamini wanatoboa kwa akina Pogba.
Ufaransa vs Argentina
“Ufaransa wamemaliza wakiwa na pointi saba (7) kutoka kwenye kundi lao wakiwa ni vinara wa Kundi C lakini kiwango chao hakiakisi pointi walizopata, walipata matokeo kwa mbinde na timu yao bado haijaungana pamoja Pogba, Kante, Griezmann bado hakuna umoja katika eneo lao la katikati.
“Wakongwe kama Frank Leboeuf amesikika mara kadhaa akielezea kutofurahishwa na kiwango kinachooneshwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakionekana kutojitoa vile inavyotakiwa
“Argentina wao wamepita kwa mbinde mbele ya Nigeria bao la Marcos Rojo ndio limewapeleka Argentina hatua ya 16 bora. Huwa wanabadilika kadiri wanavyosogea hatua za mbele na mpinzani wanaekabiliana nae.
“Diego Maradona aliwawashia moto wachezaji wa Argentina kabla ya mechi yao dhidi ya Nigeria kwa kuwaambia waheshimu jezi wanayoitumikia ambayo inaheshima kubwa iliyowekwa na magwiji waliotangulia akimaanisha kwamba, Argentina kama taifa wameshashinda ndoo ya dunia mara mbili na hiyo ni heshima tosha kwa kizazi hiki ambacho bado hakijaifanyia lolote Argentina.
“Bahati nzuri nilikuwepo kwenye mechi yao dhidi ya Nigeria na nikishuhudia matukio kadhaa ambapo kulikuwa na maelekezo yanatoka uwanjani kwenda benchi la ufundi. Hata baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi mara kadhaa Messi alionekana kuwasiliana na watu wa benchi la ufundi.
“Mabadiliko ya kumuingiza Kun Aguero ilionekana wazi yalikuwa ni mawazo ya Messi hii inaonesha hakuna umoja kwenye mambo kadhaa.
“Kama walikaa chini kwa siku hizi baada ya kufuzu 16 bora na kumaliza tofauti zao, Argentina ni timu yenye wachezaji wengi wazoefu na wenye uwezo wakiungana kwa pamoja na kucheza kama timu sioni wakizuiwa na Ufansa. Watapata matokeo na kufuzu hatua inayofuata.
Uruguay vs Portugal
“Ni mechi nyingine kubwa ambayo inakutanisha timu mbili zenye historia nzuri sana, Portugal ni bingwa wa Euro, Uruguay ina wachezaji wenye uzoefu kama Cavani, Suarez, Godin, hadi sasa hawajaruhusu goli lakini pengine kutokana na kundi walilokuwepo kutokuwa na ushindani mkubwa sana.
“Hawakuruhusu goli mbele ya Misri, Saudi Arabia na Urusi, wameingia hatua ya 16 bora wanaanza kupata changamoto ya moja kwa moja kutakiwa kumzuia Ronaldo, Quaresma wasifunge wakitoka bila kufungwa ndio watatakiwa kujipiga vifua.
“Ni mchezo mgumu ambao naiona Portugal itajaribu kutumia style yao waliyoitumia kwenye Euro ya kucheza bila kupewa nafasi lakini mwisho wa siku wanasogea kama kinyonga na unawakuta fainali.
“Natamani na ningependa kuona Messi na Ronaldo wakutane robo fainali kupambana na mmoja akate ngebe za mwenzake.